Magazetini: Kura ya Brexit kuamua hatimaya Uingereza na EU
15 Januari 2019Tukianza na gazeti la Mannheimer Morgen, kuhusu Brexit mhariri anaandika:
"Wakati tukielekea katika suluhisho linalohitajika , tatizo halipo kwa Umoja wa Ulaya , badala yake ni utekelezaji wa kisiasa wa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May . Masuala ya uzalendo , kujifaharisha si mambo yanayoweza kutosheleza na kuwafanya watu kuamini. Na kwa uwazi watu wangeweza kusema hatua hii ya Brexit inaleta uharibifu mkubwa kwa nchi yetu."
Mhariri wa gazeti la Oberhessische Presse anaandika kuhusu Brexit kuwa Umoja wa Ulaya pia unahitaji mabadiliko: Mhariri anaendelea:
"Wiki chache kabla ya uchaguzi wa bunge la Ulaya kuna hatari ya mataifa wanachama kutumbukia katika mparaganyiko, kwa kuwa uchaguzi huo unataka kuutupa mkono Umoja huo. Mamilioni ya watu katika nchi nyingine za Umoja wa Ulaya watafahamu hivi sasa, kwamba EU ni jinamizi la umangimeza, ambapo wananchi wake wanawekewa tu maelekezo yasiyostahili , na kwamba yale matamko ya mara kwa mara ya wanasiasa ya kwamba kila kitu kiko sawa , sio kweli.
Si kila kitu kinakwenda vizuri katika Umoja wa Ulaya, na hilo linaelezewa pia na wabunge wa Umoja huo, hali ambayo inaifanya Uingereza kutotaka pia kubakia katika Umoja huo. Umoja wa Ulaya mhariri anaandika, unahitaji mabadiliko na hili ni suala gumu."
Kuhusu suala la mzozo wa kidiplomasia kati ya Uturuki na Marekani, mhariri wa gazeti la Freie Presse anaandika:
"Hadhi ya Marekani inavurugika kunapotokea mara suala hili mara lile katika mashariki ya kati. Marekani ambayo hadi sasa ni nchi pekee yenye nguvu inachukua hatua nusu nusu katika kutekeleza jukumu lake katika kila uamuzi kutoka pale rais atakapoandika katika ukurasa wa Twitter hadi mara nyingine. Baadhi katika eneo hilo la mashariki ya kati wanamatumaini , kwamba huenda hakutakuwa na kitu chochochte kitakachotokea hadi wakati mwingine uchaguzi wa Marekani utakapomalizika."
Nalo gazeti la Nueremberger Nachrichten linaandika kuhusu maandishi wa rais Trump katika ukurasa wa Twitter. Mhariri anaandika:
"Donald Trump kwa mara nyingine tena amefanikiwa, kwa maandishi katika ukurasa wa Twitter kuiweka Uturuki ambayo ni mwanachama wa NATO katika mapambano dhidi yake, nafasi yake kama mpatanishi katika mashariki ya kati ameishusha na wakati huo huo nafasi ya Urusi nchini Syria kuiimarisha. Trump anataka kuyaondoa majeshi yake , lakini wakati huo huo aweze kupambana na wanamgambo wanaojiita Dola la Kiislamu pamoja na ushawishi wa Iran. Hali hii inaharibu sifa ya marekani katika mashariki ya kati."
Kwa muhtasari hayo ndio yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mahriri: Yusuf, Saumu