Magazetini: Theresa May anusurika kura ya kutokuwa na imani
13 Desemba 2018Mhariri wa gazeti la Fuldaer Zeitung likiandika kuhusiana na kura hiyo ya kutokuwa na imani na waziri mkuu Theresa May anaandika:
Uingereza na Ulaya zinaweza sasa kushusha pumzi. Kwa mtafaruku wote uliotokea katika siasa za ndani nchini Uingereza mwanamke kiongozi Theresa May bado anaendelea kubakia katika ofisi ya waziri mkuu katika mtaa wa Downing namba 10. Katika kikundi cha wabunge wa chama cha Conservative ambao hawapendelea njia anayochukua May katika suala la Brexit, hofu ilikuwa kubwa, kwamba nchi hiyo katika wakti huu mgumu inaweza kutumbukia katika hali ya kukosa kiongozi. Wingi uliowezesha May kushinda kutoka katika kundi lake ni wa kutia moyo. Haikupatikana theluthi mbili ya wabunge ambao hawataki abakie katika madaraka. Wakati mwingine matokeo kama hayo yanaweza kumlazimisha waziri mkuu kujiuzulu. Lakini huu si wakati wa kawaida mjini London. Kizungumkuti kwa May, kwamba bungeni hana wingi kwa ajili ya mkataba na Umoja wa Ulaya, hilo bado halijaondolewa na ushindi wa jana. Lakini uungwaji wake mkono unatosha kuweza kuendelea kujaribu kufikia makubaliano baina ya London na Brussels, kwa njia yoyote ile ili kuweza kupata wingi kwa ajili ya makubaliano ya Brexit. May ameonesha , kwamba ni imara na mwanamke wa shoka kuliko wakosoaji wake walivyofikiria.
Gazeti la Volksstimme la mjini Magdeburg likiandika kuhusu kura hiyo ya kutokuwa na imani bungeni jana mjini London, linaandika:
Imeonekana, Theresa May anaweza pia kushinda. Wabunge wakorofi wa chama cha Conservative , Tories, ambao walitaka kumfurusha kwa kutumia kura ya kutokuwa na imani nae, wameshindwa. May anaendelea kuwa madarakani kama kiongozi wa chama pamoja na waziri mkuu. Pamoja na hayo kwa kiongozi huyo hii ni ushindi wa taabu sana. Unapoanza mkutano wa Umoja wa Ulaya leo , anaonekana May baada ya ziara yake katika miji mikuu ya mataifa ya Ulaya kwamba uwezo wake wa upatanishi umepunguzwa. Mataifa ya Ulaya hayako tayari kuidhinisha hatua ya kubadilisha suala la mpaka wa Ireland ya kaskazini . Huenda mabadiliko kidogo ya lugha tu ndio huenda yanawezekana. Kwa jumla waziri mkuu hatakuwa na uwezo wa kubadili hali ya kupinga makubaliano hayo ya Brexit.
Mhariri wa gazeti la Rheinpfalz la mjini Ludwigshafen akiandika kuhusu shambulio la kigaidi mjini Strasbuorg anaandika:
Hapa Ujerumani huenda pengine baadhi ya watu walifikiri, kwamba ugaidi wa wapiganaji wa jihadi umekwisha, tangu pale kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria kwa kiasi kikubwa waliposhindwa. Nchini Ufaransa hakuna anayefikiria hivyo. Shambulio katika mji wa Strasbourg ni la tatu mwaka huu katika ardhi ya Ufaransa, na la tano katika wakati wa utawala wa rais Emmanuel Macron. Katika utafiti wa kituo cha tathmini ya ugaidi nchini Ufaransa kati ya mwaka 2013 na 2016 nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa zaidi na mashambulizi ya aina hiyo duniani. Katika nchi hiyo mtandao wa wana jihadi uko imara zaidi, ndani na nje ya nchi hiyo. Watafiti wanasema kuna Wafaransa maelfu kadha ambao wako tayari kufanya mashambulizi.
Bado katika mada hiyo mhariri wa gazeti la Suedkurier anaandika:
Mtu huyo alikuwa anafahamika na polisi na ana rekodi ya uhalifu. Yumo katika orodha ya Waislamu hatari wenye itikadi kali. Alipaswa kukamatwa, lakini maafisa hawakumpata na sasa ndio wanamtafuta. Baada ya shambulio mjini Strasburg linarejea tena swala la zamani likiwa na dharura mpya. Kwa nini mataifa ya kidemokrasia yanashindwa kufawajibu wao kila wakati , wahalifu kama hao kuwazuwia , nchini Ufaransa na hata hapa Ujerumani?
Nae mhariri wa gazeti la Emder Zeitung anazungumzia kuhusu mkutano wa Umoja wa mataifa wa mazingira nchini Poland. Mhariri anaandika.
Kesho unamalizika mkutano huo. Kwa bahati mbaya, kunakuja kile ambacho hadi sasa tumekisikia katika mkutano wa mazingira, kile tunachokifahamu kila mmoja. Baada ya miito ya kina kwamba ni muhimu kiasi gani kufikia makubaliano yenye manufaa, inashindikana kwa mara nyingine tena kupata ushauri imara. Masuala muhimu yanayoleta vizuwizi bado hayajatatuliwa, alisema katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres jana. Hali hii si nzuri kabisa. Mtu hapaswi hata hivyo kukata tamaa, lakini ni wazi kwamba hatari ni kubwa, kwamba jumuiya ya kimataifa bado ina nafasi ya mwisho, kuzuwia mabadiliko ya tabia nchi ambayo hayajazuiliwa na yameachwa kusambaa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Josephat Charo