1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini: Uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki

Sekione Kitojo
21 Agosti 2018

Wahariri wa  magazeti  ya  Ujerumani wamejishughulisha leo(21.08.2018)na mada kuhusu uhusiano kati ya Ujerumani  na Uturuki, kuondolewa kwa marufuku  ya  kusafiri kwa Mesale Tolu raia wa Ujerumani kwenda Uturuki.

https://p.dw.com/p/33SjX

Tukianza  na  gazeti  la  Rhein-Neckar-Zeitung la  mjini Heidrlberg  kuhusu  uhusiano  kati  ya  Uturuki  na Ujerumani, mhariri  anaandika  kwamba rais  wa  Uturuki Erdogan kwa  muda  wa  miaka  miwili  ameweza sio  tu kuondoa utawala  wa  kisheria  nchini  mwake, bali  pia ameharibu  uchumi  wa  nchi  hiyo. Mhariri  anaendelea:

"Uchumi  uliokuwa  unakua  kwa  kasi  umefikia  mwisho. Kile pekee  ambacho  kinaendelea  kuongezeka  nchini Uturuki ni kodi. Katika  hali  hii kile  ambacho  dikteta  huyo anachotaka  ni  msaada  wa  fedha  kutoka  Ujerumani. Ndivyo  anavyotaka  pia kiongozi  wa  chama  cha  SPD Andrea Nahles. Na  ndio sababu  huenda  Erdogan anataka  kumwachilia  huru mmoja  kati  ya  mateka   wake wengi. Mwandishi  habari  Mjerumani Mesale Tolu, ambaye amefunguliwa  mashitaka  ya  bandia  kwamba  ni  msaliti."

Gazeti  la  Stuttgarter Nachrichten  linazungumzia  pia uhusiano  kati  ya  Ujerumani na  Uturuki  kwa  kuandika kwamba uhusiano  huo  ambao  ni mbaya  umeendelea kuwa  mbaya zaidi.  Na  ndio  sababu  unajitokeza  wazi mwelekeo  wake, vile  Ujerumani  inavyotaka. Mhariri anaadika:

"Na kuna  mwelekeo  mmoja  tu. Uturuki  inabakia  kuwa mshirika  wetu  muhimu kutokana  na  uhusiano  mkubwa wa  kijamii pamoja  na  maslahi  ya  pamoja  ya  kiusalama. Hii  haina  maana  kwamba tunapaswa  kuacha  kila  aina ya  uwezekano wa  uchokozi  ama  kupuuzia  kila  kashfa, ambayo  uongozi  wa  Uturuki  unajaribu  kila  wakati kuendesha mtandao  wa  ushawishi  wa  matukio  ya kihalifu  nchini  Ujerumani. Lakini  kwa  kuwa  kumekuwa na  uhusiano  wa  karibu ambao ni  karibu  na  kuwa  katika familia  moja, ni  lazima  tumuangalia  ndugu katika  hali nzuri  na  mbaya . Kwa  hiyo  majadiliano  ni  muhimu kuendelea."

Katika  suala  la  kuachiliwa  huru Mesale Tolu mwandishi habari  wa  Ujerumani  nchini  Uturuki , mhariri  wa  gazeti la Südwest Presse  la  mjini  Ulm anaandika:

"Erdogan  kwa  hivi  sasa  anaihitaji  Ulaya. Mchezo  wake wa  kujitoa  muhanga  dhidi  ya  Marekani  unaipeleka  nchi yake  katika  mzozo  hatari. Bila  ya  uwekezaji, fedha  za kodi na  mikopo  kutoka  Ulaya zinatishia  mtikisiko  katika sarafu  ya  nchi  hiyo kutumbukia  katika  hali  ambayo haitaweza  kudhibitika. Na  hali  hii  haina  maslahi  kwa Uturuki  ama  Umoja  wa  Ulaya. Uturuki  chini  ya  rais Erdogan  inabaki  kuwa  mshirika  asiyetabirika. Anatumia wafungwa  wa  kisiasa  katika  masuala  ya  siasa na kufunganisha na  masuala  ya  sheria. Mambo yote  hayo anayatumia  kama  nyenzo  zake."

Kuhusu  mada  ya  mwisho  Ugiriki  kupatiwa  msaada zaidi, licha  ya  awamu ya  mwisho ya msaada  ukikaribia kumalizika. Mhariri  wa  gazeti  la Volksstimme  la  mjini Magdenburg  akizungumzia kuhusu  suala  hilo  anaandika:

"Licha  ya  kiasi  kikubwa  cha  mkopo na  hatua  madhubuti za  kurejesha  mkopo  huo, bado  Ugiriki imo  katika matatizo. Kwa  nini  nchi  hiyo  inataka  kufutiwa  deni  lake ifikapo  mwaka 2032. Na vipi  nchi  hiyo inataka  katika muda wa  miaka 40 kutowajibika  kuhusu  masuala  ya  riba na ziada katika   bajeti yake?. Kwa  hivi  sasa  kila  mmoja anamatumaini tu  kwamba  soko  la  fedha  linaendelea kuwa  na  imani  na  sarafu  ya  euro, na  kutoiacha  Ugiriki kuporomoja."

Hayo  ndio  aliyoweza  kutukusanyia  Sekione  Kitojo kutoka  kwa  baadhi  ya wahariri  wa  magazeti  ya Ujerumani.

Mwandishi:  Sekione  Kitojo /  Inlandspresse

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman