1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mageuzi ya Arabuni yatawala Davos

25 Januari 2013

Viongozi kadhaa wa mataifa ya Kiarabu wanazungumza kwenye mkutano wa jukwaa la kiuchumi la Davos, wakijikita kwenye mageuzi nchini mwao baada ya vuguvugu la umma kuziangusha tawala za muda mrefu kwenye eneo hilo.

https://p.dw.com/p/17RFe
Mwanzilishi na Rais wa Jukwaa la Uchumi Duniani.
Mwanzilishi na Rais wa Jukwaa la Uchumi Duniani.Picha: dapd

Seneta John McCain wa Marekani amepangiwa kushiriki kwenye jopo la mustakabali wa Syria, taifa la Kiarabu ambalo hadi sasa linaendelea na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mfalme Abdullah II wa Jordan anazungumza mbele ya jopo la wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa duniani, ikiwa ni siku moja tu baada ya uchaguzi wa bunge nchini mwake kuonesha kwamba vyama vinavyouunga mkono utawala wake na wafanyabiashara wameshinda.

Uchaguzi huo ulichukuliwa kama hatua za kuunga mkono demokrasia za Mfalme Abdullah II lakini umekosolewa na kususiwa na Chama cha Udugu wa Kiislamu, ambalo ndilo kundi kubwa la upinzani nchini humo, kinachotaka mageuzi makubwa na ya jumla-jamala.

Mawaziri wakuu wa Misri, Lebanon, Libya, Tunisia na Palestina wanatarajiwa kuvutia washiriki wengi wa jukwaa hilo la Davos, ambalo linawakutanisha pamoja wanasiasa, wasomi, wafanyabiashara na watu wa fani mbalimbali kujadiliana mustakabali wa dunia.

Ban Ki-moon aonya 'ugoigoi' wa dunia kwa Syria

Hapo jana Alhamis (tarehe 24 Januari), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alitumia ziara yake ya Davos kutoa tena wito kwa wanachama wa Baraza la Usalama kusuluhisha tafauti zao na kutafuta suluhisho la vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akizungumza mjini Davos.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akizungumza mjini Davos.Picha: dapd

Ban alisema kwamba utakuwa "ukiukaji majukumu" wa chombo hicho kikuu duniani kama kitashindwa kuungana dhidi ya mgogoro huo ambao umeshagharimu maisha ya watu zaidi ya 60,000 hadi sasa.

"Litakuwa ni jambo la lazima kwa Baraza la Usalama kuukwamua mkwamo huu, na kutafuta umoja utaochukua hatua ya manufaa," Ban aliiuambia mkutano huo wa kila mwaka nchini Uswisi.

"Njia hii tuliyochagua ya kuziacha pande hasimu zipigane, ya kujitenga na uharibifu wa Syria licha ya athari yake kubwa kwa eneo zima, ina gharama kubwa sana na wala haivumiliki," aliongeza.

"Huko ni ugoigoi kwa dhamana yetu ya msingi ya kuilinda dunia na watu wake. Dunia, na juu ya yote Baraza la Usalama, lazima litimize wajibu wake huo."

Misri yaahidi kusonga mbele

Waziri Mkuu wa Misri, Hisham Qandil, pia amezungumzia juu ya haja ya nchi yake kuelekeza makini yake kwenye uchumi katika wakati huu ambapo kipindi cha mpito cha kisiasa kinasonga mbele, ikiwa ni miaka miwili baada ya kuanguka kwa Hosni Mubarak.

Waziri Mkuu wa Misri, Hisham Qandil.
Waziri Mkuu wa Misri, Hisham Qandil.Picha: Reuters

"Miaka miwili iliyopita, watu wa Misri walisimama kidete dhidi ya dikteta wa Misri, na ndani ya siku 18 tu walimwangusha Mubaraka na utawala wake na kuanza enzi mpya," Qandila aliwaambia waandishi wa habari.

Alisema kwamba kufuatia uchaguzi wa rais na kura ya maoni ya katiba, sasa Misri itafanya uchaguzi wa bunge ndani ya kipindi cha miezi miwili au mitatu kutoka sasa.

"Baada ya hapo tutakuwa tumekamilisha kipindi cha mpito kwa kuwa na taasisi zote za kidemokrasia. Lakini kwa upande mwengine, tuna kazi kubwa ya kuufufua na kuujenga uchumi," alisema Qandil.

Umoja wa Ulaya wajadiliwa

Ulaya imekuwa kiini chengine cha mijadala mjini Davos wiki hii, ambapo Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, hapo siku ya Alhamis alisisitiza kwamba hajaiacha mkono Ulaya, hata baada ya kuweka wazi mipango yake ya kuitisha kura ya maoni kuwapa fursa Waingereza ya kuamua juu ya kuendelea kuwa wanachama wa Umoja huo.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron akizungumza mjini Davos.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron akizungumza mjini Davos.Picha: Reuters

Mkuu wa Benki ya Ulaya, Mario Draghi, anatarajiwa kulihutubia jukwaa hilo leo Ijumaa juu ya "Mustakabali wa Sarafu ya Euro", ambapo wataalamu wa uchumi na wafanyabiashara watajadiliana juu ya njia za kuufufua uchumi wa dunia.

Tayari mchumi wa ngazi za juu kutoka Marekani, Barry Eichengreen, ameshasema kwamba kutulia kwa sasa kwa hali ya kifedha kwenye kanda ya euro, hakumaanishi kwamba hali ni shwari. Eichengreen ameonya kwamba mwaka 2013 utakuwa mwaka mwengine mbaya kifedha kwa eneo hilo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman