1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mtarajiwa Magufuli apewa cheti

30 Oktoba 2015

Rais mteule wa Tanzania John Magufuli amekabidhiwa rasmi cheti cha ushindi lakini hali inaendelea kuwa ya wasiwasi kufuatia madai ya upinzani kuwa uchaguzi uligubikwa na udanganyifu. Zanzibar nako bado hakijaeleweka

https://p.dw.com/p/1Gx4K
Tansania Wahlkampf - John Pombe Magufuli & Jakaya Kikwete
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Said

Magufuli alimshinda mpinzani wake mkuu kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo - Chadema, ambaye pia aliviwakilisha vyama vingine vitatu vinavyounda muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA - Edward Lowassa, kwa asilimia 58 ya kura dhidi ya asilimia 40 za Lowassa, waziri mkuu wa zamani wa Tanzania aliehamia upinzani mwezi Julai, baada ya kuenguliwa kwenye kinyanganyiro cha kuogombea nafasi hiyo kuitia chama cha mapinduzi.

Akimkabidhi cheti hicho siku ya Ijumaa mbele ya rais anaemaliza muda wake Jakaya mrisho Kikwete, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Tanzania NEC, Jaji Damian Lubuva, alisema cheti hicho kinakabidhiwa kwa mujibu wa sheria kwa rais aliechaguliwa kidemokrasia pamoja na makamu wake. Jaji Lubuva kabla ya kumkabidhi cheti hicho Dk. Magufuli, alianza kwa kurudia kuyasoma matokeo yaliyompa ushindi kwenye uchaguzi huo kwa ngazi ya urais.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vingine vilivyosimamisha wagombea kwenye uchaguzi huo, mgombea wa chama cha ACT - Wazalendo Anna Mghwira alikubali matokeo yaliyompa ushindi Magufuli, na kumtaka asimamie ahadi ya mabadiliko, ambayo vyama vyote viliitumia kwenye kampeni hizo.

Mgombea wa Chadema na Ukawa Edward Lowassa.
Mgombea wa Chadema na Ukawa Edward Lowassa.Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

"Ninamuomba rais mteule Dk. Magufuli, asimamie mabadiliko ambayo ni matamanio ya Watanzania wengi. Jambo la kwanza ambalo ndiyo msingi wa mabadiliko yote ni kuhakikisha kuwa tunapata katiba mpya itakayotokana na maoni ya wanachi na mambo mengine yatafuata," alisema Bi Mghwira.

Aliongeza kuwa Magufuli ana wajibu wa kusimamia umoja wa kitaifa, usawa na kijinsia kati ya wanaume na wanawake, kusimamia serikali na mfumo wa uchumi ili kuondoa umaskini kwa kuwa Tanzania na Watanzania siyo maskini.

Lowassa asusia hafla ya kukabidhi cheti

Mgombea mkuu wa upinzania Edward Lowassa pamoja na wagombea wengine - Hashim Rungwe wa chama cha Chauma na Maximilana Lymo wa chama cha TLP hawakuhudhuria hafla hiyo ya kukabidhiwa cheti cha ushindi kwa Dk. Magufuli, ambaye alitimiza miaka 56 siku alipotangazwa mshindi wa nafasi hiyo ya juu kabisaa nchini Tanzania.

Lowassa na chama chake cha Chadema pamoja na vyama washirika walikataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi huo, kwa madai kuwa kura zilichakachuliwa na tume ya uchaguzi NEC, ili kumpa ushindi rais mteule Dk- Magufuli. "Tunalikataa jaribio hilo la kuwapora Watanzania haki yao ya kimokrasia, linalofanywa na tume ya uchaguzi kwa kutangaza matokeo ambayo siyo ya kweli," Lowassa aliwambia wandishi habari.

Utulivu waendelea kutawala kaskazini

Mwandishi wa DW mkoani Arusha ameripoti kuwa hali ya utulivu imeendelea kushuhudiwa katika eneo la kaskazini mwa Tanzania, ambalo ni ngome kuu ya chama cha upinzani cha Chadema, bila kuwepo na matukio yoyote ya vurugu licha ya vijana kujikusanya makundi wakijadili matokeo ya urais.

Katika mji wa Arusha jeshi la polisi limeimarisha usalama kwa kufanya dorio kuzunguka katika viunga vya mji kwa lengo la kukabili lolote linaloweza kujitokeza. "Sehemu kubwa ya mji imetulia na kuna hali ya simanzi hivi katika vijiwe na mitaa yenye wafuasi wengi wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema na vyama vingine vya upinzani," ameripoti mwandishi wetu Charles Ngereza.

Ris wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein.
Ris wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein.Picha: DW/M. Khelef

Wengi wa makada na wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema wanasema kuwa wanasubiri masimamo wa mwisho wa viongozi wao kuhusu nini kitaendelea baada ya viongozi wa juu wa chama hicho na mgombea urais kugomea matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.

Zanzibar bado si shwari

Hali inazidi kuwa ya mashaka katika visiwa vyenye mamlaka yake vya zanzibar, ambako matokeo ya uchaguzi yalifutwa na mwenyekiti ya tume ya uchaguzi visiwani humo ZEC, Jecha Salum Jecha, kwa madai ya ukiukaji wa taratibu za uchaguzi. Chama cha upinzani visiwani humo - Chama cha Wananchi CUF, kilisema kilishinda uchaguzi huo, na kudai kuwa hatua ya kufutwa kwa matokeo ilikuwa njama ya chama tawala CCM kukwepa kukubali kushindwa.

Polisi visiwani humo imewakamata vijana kadhaa waliokuwa wamezuwia barabara kupinga kufutwa kwa uchaguzi huo. Kamishna wa polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame hakutoa idadi kamili ya waliokamatwa lakini alisema kwa njia ya simu kwamba hali ilikuwa tulivu, ambapo askari polisi wanafanya doria mitaani.

Marekani na Uingereza zilisema zilishtushwa na uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya Zanzibar. Katibu Mkuu wa chama cha CUF na mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho, Maalimu Seif Sharif Hamad aliwataka wafuasi wake kuwa watulivu wakati wanautafutia ufumbuzi mgogoro huo, huku akiwatolea mwito rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete na Ali Mohamed Shein wa Zanzibar, kuweka mbele maslahi ya Tanzania na Zanzibar kwa kuingilia kati na kutatua suala hilo.

Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na mashirika mengine ya kimataifa walitoa taarifa wakisema wana wasiwasi na uamuzi wa Zanzibar, baada ya hapo awali kundi la waangalizi hao kuthibitisha kuwa mchakato wa uchaguzi ulikuwa wa uwazi.

Mgombea wa chama cha CUF Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Mgombea wa chama cha CUF Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.Picha: DW/M. Khelef

"Demokrasia na amani nchini Tanzania viko hatarini," ilisema taarifa ya waangalizi wa kimataifa, wakiwemo Umoja wa Afrika inayoongozwa na rais mstafu wa Msumbiji Armando Guebuza, jumuiya ya madola iliyoogozwa na rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan.

Wanasheria waonya

Mwandishi wetu wa Zanzibar Salma Said ameripoti kuwa chama cha Wanasheria wa Zanzibar ZLS, kimeitaka tume ya uchaguzi ya Zanzibar kutengua maamuzi ya mwenyekiti wa tume Jecha Salum Jecha kufuta uchaguzi kwa sababu tamko lake linakwenda kinyume na sheria, na kumtaka rais Shein kuunda tume ya kumchunguza mwenyekiti huyo na achukuliwe hatua stahiki.

Wanasheria hao wamemtahadharisha pia rais Shein kuwa muangalifu asije kutumbukia kwenye mtego ambao utamuweka katika vitabu vya historia kama kiongozi alieitumbukiza Zanzibar kwenye mgogoro wa umuagaji damu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga

Mhariri: Saumu Yusuf