Magufuli aongoza Watanzania kumuaga Mkapa
28 Julai 2020Mbele ya umati mkubwa wa watu waliofika katika uwanja wa uhuru kushuhudia shughuli hiyo, Rais Magufuli ameshindwa kujizua wakati alipokuwa akihutubia taifa kuhusu maisha jumla ya Rais Mkapa aliyefariki duniani usiku wa kuamkia Ijumaa (Julai 23).
Kando ya kummwagia sifa kiongozi huyo aliyehudumu kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kabla ya kuhitimisha kwa mihula miwili yake ya urais (1995-2005), Rais Magufuli alijikuta akikatishakatisha kwa muda hotuba yake kutokana na hisia kali za majonzi.
"Ni ukweli usiopingika kwamba nchi yetu, Afrika na dunia imeondokewa na mtu muhimu sana," alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alimwelezea kiongozi mwenzake huyo kama mtu aliyetoa mchango mkubwa kuanzia katika siasa za nyumbani mpaka katika duru za kimataifa.
"Kutokana na mchango mkubwa katika maisha yake binafsi kwa taifa kwa ujumla, Rais Mkapa ataendelea kuwa shujaaa wake daima," alisema Rais Magufuli.
Burundi wamlilia Mkapa
Shughuli hiyo ya kitaifa ya kuuaga mwili wa kiongozi huyo ilihudhuriwa na viongozi wote wa kitaifa, wakati Burundi ikiwakilishwa na waziri wake mkuu, Jenerali Alain Guilaume, aliyewasili nchini tangu jana.
Mabalozi na watendaji wengine wanaofikia kwa pamoja 41 waliziwakilisha nchi zao kwenye shughuli hiyo iliyoanza asubuhi na kumalizika saa sita mchana.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu wa Burundi, Jenerali Guilaume alisema kifo cha Mkapa ni pengo kubwa katika eneo la Maziwa Makuu hasa kwa namna alivyokuwa mshirika muhimu katika kutatua migogoro iliyoikumba eneo hilo.
Mwili wa Rais Mkapa umesafirishwa mchana huu kuelekea Wilayani Masasi na kisha kusafirishwa moja kwa moja katika kijiji alichozaliwa cha Lupaso kwa ajili ya kusubiri maziko yanayotarajiwa kufanyika Jumatano (Julai 29) kuanzia saa 8:00 mchana.
Rais Mkapa ameondoka katika wakati ambapo Tanzania ikiwa kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu na mara nyingi uwepo wake ulisadia siyo tu kuchangamsha siasa za ushindani, bali pia uliimarisha utulivu ndani ya chama chake cha CCM.
Rais Magufuli amehaidi kuyalinda yale yote yaliyoasisiwa na kiongozi huyo ikiwamo kuusimamia vyema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, alama kubwa ambayo imekuwa ikiudumisha uhalali wa miongo zaidi ya sita ya taifa hilo la Afrika Mashariki.
George Njogopa/DW Dar es Salaam