Rais John Magufuli wa Tanzania asema taifa hilo si maskini
1 Agosti 2019Rais Magufuli ambaye leo amezindua jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere amesisitiza kwamba, Tanzania inapaswa kujiamulia mambo yake. Amesema wapo watu waliojaribu kuaminisha dunia kwamba Tanzania ni taifa maskini na hivyo haliwezi kufanya mambo yake bila kutegemea usaidizi.
Ameeleza, kudhihirisha kwamba Tanzania siyo maskini na iko tayari kujiamulia mambo yako, tayari inatekeleza miradi mikubwa ya kimaendeleo ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa(SGR), mradi wa kuzalisha umeme wa mto Rufiji yaani Stiagles Gorge pamoja na uamuzi wa serikali yake kuhamia Dodoma.
Ama, Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kuelezea hali ya uchumi wa taifa akisema mwelekeo ni mzuri na kuitaja Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa machache barani afrika ambayo uchumi wake unakuwa kwa asilimia saba.
Awaonya watendaji wazembe
Pia, alionya kuhusu watendaji wazembe huku pia awanyoshea kidole wale aliowaita mafisadi. Amesema zama zao sasa zimekwisha na serikali imebana mianya yote waliyokuwa wakitumia kufuja fedha.
Kuhusu jengo hilo lililozinduliwa linatajwa kuwa la kisasa likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka. Kwa maana hiyo kwa kuunganisha majengo yote matatu uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuwahudumia abiria milioni nane kwa mwaka.
Uzinduzi huo umefanyika katika wakati ambapo shirika la ndege la Tanzania likipata uhai mpya kwa kupatiwa ndege nane wakati nyingine tatu zikitarajiwa kuwasili nchini mwezi disemba.
Uzinduzi wa jengo hilo huenda pia ukaongeza idadi ya watalii wanaokuja Tanzania hasa wakati huu ambapo vivutio vya utalii vikitangazwa zaidi, licha ya kuwa ni kivutio cha mashirika mengi ya ndege ya kigeni kutua katika uwanja huo na kufanya shughuli zao kwa njia bora zaidi.
Mwandishi: George Njogopa, DW, Dar Es Salaam