Mahakama Afrika Kusini yasikiliza kesi ya Zuma kugombea
10 Mei 2024Mahakama ya juu nchini Afrika Kusini imeanza kusikiliza hoja za kisheria ikiwa rais wa zamani Jacob Zuma anaweza kuwania ubunge. Matokeo yakesi hiyo huenda yakaathiri pakubwa uchaguzi mkuu wa kitaifa utakaofanyika Mei 29 na kusababisha pia ukosefu wa usalama endapo atashindwa.
Kesi hiyo inatokana na uamuzi wa mwezi Machi wa tume ya uchaguzi, iliyomzuia Zuma kuwania ubunge kwa msingi kwamba Katiba inakataza mtu yeyote aliyepewa adhabu ya kifungo jela cha miezi 12 kuwania nafasi ya bunge.
Soma pia: Tume ya Uchaguzi Afrika Kusini yaukatia rufaa uamuzi wa kumruhusu Zuma kugombea
Zuma mwenye umri wa miaka 82, ambaye alilazimika kujiuzulu kama rais mwaka 2018 na kufungwa jela mwaka 2021, ametofautiana na chama tawala cha African National Congress ANC na amekuwa akikipigia kampeni chama chake kipya cha uMkhonto we Sizwe (MK).
Utafiti wa kura za maoni unaashiria kuwa ANC itapoteza uungwaji mkono mkubwa baada ya kuwa madarakani kwa miaka 30. Chama cha MK kinatoa kitisho kwa ANC haswa katika jimbo la nyumbani kwa Zuma la KwaZulu Natal.