Mahakama Kongo yamwachilia mshauri wa zamani wa Rais
23 Agosti 2023Mahakama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imemwachilia huru mshauri wa zamani wa rais aliyetuhumiwa kwa uhaini na kuwaunga mkono waasi.
Fortunat Biselele, ambaye alikamatwa mwanzoni mwa mwaka huu na kuzuiliwa kabla ya kuwachiliwa huru kwa muda mnamo Julai 22, pia alikuwa ameshitakiwa kwa kuwa na mawasiliano na Rwanda.
Wanaharakati waonya ukandamizaji wa Kongo: HRW: Serikali ya Kongo yakandamiza wapinzani kuelekea uchaguzi
Wakili wake, Richard Bondo, amesema mahakama ya Kinshasa imemfutia mashitaka yote.
Sakata hilo lililipuka baada ya video kuibuka ya Biselele akizungumzia mahusiano ya kiuchumi kati ya Rais Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame.
Mahusiano kati ya majirani hao wawili, ambayo yalionekana kuelekea kurekebishwa wakati Tshisekedi alichukua madaraka Januari 2019, yameharibika pakubwa tangu kuibuka tena kwa uasi wa M23 mashariki ya Kongo.