1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama nchini Misri yasema kamwe haitabadili uamuzi wake

MjahidA9 Julai 2012

Mahakama kuu ya kikatiba nchini Misri imesema kuwa uamuzi wake wa kufutiliwa mbali kwa bunge nchini humo mwezi uliopita kamwe hautabadilika

https://p.dw.com/p/15UMI
Mahakama ya kikatiba nchini Misri
Mahakama ya kikatiba nchini MisriPicha: picture-alliance/dpa

Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya rais mpya Mohammed Mursi kutoa agizo la bunge kufunguliwa tena. Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mahakama Kuu, maamuzi yoyote kutoka katika korti hiyo ni ya mwisho na yanapaswa kuheshimiwa na wala hayapaswi kukatiwa rufaa.

Shirika la habari la nchi hiyo limenukuliwa likisema kwamba korti kuu imethibitisha kuwa uamuzi wake wa kulifuta bunge hautabadilika, jambo ambalo kwa sasa hivi limeonekana kuzua utata kati ya mahakama na jeshi kwa upande mmoja na Rais Mursi kwa upande mwengine.

Jeshi liliungana na hatua ya mahakama ya kikatiba kuvunja bunge ili kujipa madaraka ya kutunga sheria nchini Misri. Mahakama hiyo ilisema ilichukua uamuzi huo kwa kuwa thuluthi moja ya bunge hilo ilichaguliwa kwa njia isiyo halali.

Hatua hii ilikikasirisha chama cha Udugu wa Kiislamu ambacho kilikuwa na wajumbe wengi katika bunge hilo.

Rais Mpya wa Misri Mohammed Mursi
Rais Mpya wa Misri Mohammed MursiPicha: Reuters

Wakili wa maswala ya katiba nchini humo Ibrahim Darwish awali alisema kwamba hatua ya Mursi huenda ikayumbisha amani na utulivu uliokuwa umeanzakuonekana nchini humo na hapa anaeleza athari zaidi ya matamshi ya Mursi.

Hatua ya spika wa bunge Saad el-Katatni kutaka kikao cha dharura kifanyike imekuja punde tu baada ya Mursi kutoa agizo la kufunguliwa tena kwa bunge baada ya mahakama kulifutilia mbali mwezi uliopita.

Kwa sasa ni watu wengi tu waliokwenda Mahakamani kutaka kujua iwapo Rais Mursi alikuwa na uwezo kisheria kuagiza bunge kufunguliwa tena licha ya mahakama kuu kulifutilia mbali.

Hata hivyo mahakama hiyo imesema itashughulikia kesi hizo baadaye huku ikisema kwamba haina uanachama na chama cocote cha kisiasa nchini humo na kwamba kazi yake ni kulinda maandishi ya katiba ya nchi.

Rais Mursi anayetoka chama cha Udugu wa Kiislamu ambacho kimekuwa katika hali ya kutoelewana na jeshi, pia alisisitiza uchaguzi wa bunge kufanyika katika siku 60 zijazo ili kuweza kupata katiba mpya ya nchi hiyo inayotarajiwa kuundwa mwishoni mwa mwaka huu.

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Reuters

Shirika la habari la AFP limesema rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kukutana na Mursi katika mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini New York mwezi wa Septemba.

Licha ya kuwa Mursi anatoka katika chama chenye kufuata siasa za Kiislamu, kuhibitishwa kwake kama rais kulileta hali ya utulivu katika utawala wa Obama baada ya kuwa na hofu kwamba jeshi lililoongoza nchi lisingekubali ushindi wa Mursi hatua iliyozua wasi wasi wa kuwa na vurugu nchini humo.

Mwandishi Amina Abubakar/AFPE/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef