Mahakama Uganda yasema Rukirabashaija aachiwe huru
5 Januari 2022Mwandishi huyo ambae ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Museven, Kakwenza Rukirabashaija alikamatwa nyumbani kwake mjini Kampala wiki iliopita akishutumiwa kutumia mitandao ya kijamii kumtusi mtoto huyo wa Rais Museven Jenerali mwenye nguvu serikalini Muhozi Kainerugaba akimtaja kuwa mnene na mkorofi. Waganda wengi wanaamini mtoto wa Museveni ndie anaeandaliwa kuchukua nafasi ya baba yake mwenye umri wa miaka 77.
Hakimu Irene Nambatya aliamuru kwamba Rukirabashaija aachiliwe bila masharti huku akiwataka kila afisa wa polisi kuzingatia amri hiyo. Wakili wa mwandishi huyo Eron Kiiza ameliambia shirika la habari la AFP kwamba alinyimwa fursa ya kuonana na mteja wake ambae alipitia mateso akiwa chini ya ulinzi huku akishindwa kufika mahakamani kujibu tuhuma za ujumbe wa kukera, kutokana na polisi kuhofia alama za mateso alizonazo mteja wake.
Msemaji wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai Charles Twiine amesema mwandishi huyo alitakiwa kushtakiwa kwa mujibu wa sheria ya kosa la matumizi mabaya ya kompyuta ambapo akikutwa na hatia anaweza kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.
Je kipi kilichomponza Rukirabashaija?
Siku ya kukamatwa kwake mnamo Desemba 28 mkosoaji huyo wa serikali ya Rais Museven alichapisha ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook ukisema Watu wenye bunduki wanavunja mlango wangu, wakisema wao ni polisi lakini hawajavaa sare.
Rukirabashaija amekuwa akikamatwa na kuteswa mara kwa mara tangu alipochapisha Riwaya yake iliokwenda kwa jina la The "Greedy Barbarian", au "Mshenzi Mroho" ambayo ilipata tuzo kutokana na kuelezea ufisadi wa hali ya juu katika nchi ya kufikirika. Mwandishi huyo pia alitunikiwa tuzo ya PEN Printer 2021 ambayo hutolewa kwa waandishi wa kimataifa waliopitia mateso kutokana na kuandika kweli.
Kiiza amesema anajua mwandishi huyo wa riwaya anazuiliwa kituo kinachoendeshwa na Kamandi ya Kikosi Maalum, ambacho ni kitengo cha kijeshi kilichokuwa kikiongozwa zamani na mtoto wa Museveni, ambacho kinashughulikia kazi maalum ikiwa ni pamoja na kumlinda Rais.
Hata hivyo msemaji wa jeshi la Uganda Flaviana Byekwaso alipopigiwa na shirika la habari Reuters anasema anahitaji kufanya mashauriano kabla kutoa maoni.
Rukirabashaija ambaye amekuwa akimkosoa Museveni na mwanae Muhozi Kainerugaba, Jenerali wa jeshi anaetazamwa na wengi kuwa anaandaliwa kuchukuwa urais kutoka kwa baba yake, aliedumu madarakani sasa kwa miaka 35, hajaruhusiwa kukutana na familia yake, wala watu wake wa karibu.
Chanzo: afp/ap