1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Watu 51 wahukumiwa kifo kwa mauaji ya wataalam wa UN

Zainab Aziz Mhariri: Lilian Mtono
30 Januari 2022

Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewahukumu adhabu ya kifo watuhumiwa 51 waliokabiliwa na kesi ya mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa waliouawa mwaka 2017.

https://p.dw.com/p/46H1d
Demokratische Republik Kongo Yumbi-Prozess
Picha: Jonas Gerding/DW

Idadi kubwa ya watu walikuwa wakifuatilia kesi hiyo mahakamani tangu ilipoanza kusikilizwa zaidi ya miaka minne iliyopita. Michael Sharp, raia wa Marekani na Zaida Catalan raia wa Sweden na Chile, walikuwa wakichunguza machafuko katika mkoa wa Kasai, chini ya Umoja wa Mataifa.

Uchunguzi wao ulijikita kwenye makaburi ya halaiki yanayohusishwa na mzozo wa umwagaji damu ambao ulikuwa umepamba moto kati ya serikali na kundi la waasi la Kamwina Msapu katika mkoa wa Kasai.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Watalamu hao wa Umoja wa Mataifa walipotea na kisha miili yao ilipatikana katika kijiji kimoja mnamo Machi 28, mwaka 2017, siku 16 baada ya kutoweka. Mtaalamu Zaida Catalan alikuwa amekatwa kichwa.

Mauaji hayo ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa yaliitikisa jamii ya wanadiplomasia na wafadhili na serikali ya Kongo imelilaumu kundi la Kamwina Msapu kwa mauaji hayo.

Waendesha mashtaka katika mahakama ya kijeshi ya Kananga walipendekeza hukumu ya kifo dhidi ya washtakiwa 51 kati ya washtakiwa 54. Watuhumiwa 22 wamehukumiwa bila kuwepo mahakamani hapo kwa sababu wametoroka kutoka nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Watuhumiwa wakabiliwa na mashtaka lukuki

Mashtaka yaliyowakabili watuhumiwa kwenye kesi hiyo ni pamoja na ugaidi, mauaji, kushiriki katika vuguvugu la uasi na kutenda uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu.

Hukumu ya kifo hutolewa katika kesi za mauaji nchini DRC, lakini hubadilika na kuwa kifungo cha maisha tangu taifa hilo lilipotangaza kusitisha kuwanyonga watu waliohukumiwa adhabu ya kifo mwaka 2003. Mahakama iliwaachia huru washtakiwa wengine wawili akiwemo mwandishi wa habari.

Kulingana na maelezo rasmi ya matukio, wanamgambo wa Kamuina Nsapu waliwaua watalaamu hao wawili mnamo Machi 12, 2017, siku ambayo walitoweka. Mnamo mwezi Juni 2017, ripoti iliyokabidhiwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ilielezea mauaji hayo kuwa yalipangwa kimakusudi ambapo huenda vikosi vya usalama vya serikali pia vinaweza kuwa vilihusika.

Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  Felix Tshisekedi
Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix TshisekediPicha: Giscard Kusema/DRC Presidential Press Service

Wakati wa kusikilizwa kesi hiyo, waendesha mashtaka walipendekeza kuwa wanamgambo walifanya mauaji hayo ili kulipiza kisasi dhidi ya Umoja wa Mataifa, ambao kikundi hicho kiliushutumu kwa kushindwa kuzuia mashambulizi dhidi yao na yaliyokuwa yakifanywa na jeshi.

Kanali Jean de Dieu Mambweni

Miongoni mwa washtakiwa wakuu ni kanali, Jean de Dieu Mambweni, ambaye waendesha mashtaka wanasema alishirikiana na wanamgambo hao, kwa kuwapa silaha. Amekana mashtaka hayo na mawakili wake wanasema kesi hiyo imepangwa mahsusi kumvika lawama kanali huyo.

Mambweni alikuwa miongoni mwa watu waliokabiliwa na hukumu ya kifo, lakini badala yake amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kukaidi amri na kushindwa kutoa msaada kwa mtu aliyekuwemo hatarini. Mawakili wake wamesema watakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo. Waliohukumiwa wanaweza kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Kijeshi ya mjini Kinshasa.

Vyanzo:AFP/https://p.dw.com/p/46Gx1