1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Haki yaanza kusikiliza kesi dhidi ya Ujerumani

8 Aprili 2024

Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ imeanza hii leo kusikiliza kesi iliyowasilishwa na Nicaragua, inayotaka Ujerumani kuacha kuipatia Israel msaada wa kijeshi na misaada mingine.

https://p.dw.com/p/4eXJR
Prüfung Israels Besatzungspolitik am Internationalen Gerichtshof in Den Haag
Picha: Robin van Lonkhuijsen/ANP/AFP/Getty Images

Haya ni kwa kuzingatia madai kwamba Berlin inasaidia vitendo vya mauaji ya kimbari na kukiuka sheria ya kimataifa ya kiutu katika vita kati ya Israel na Hamas.

Nicaragua iliyowasilisha kesi hiyo inadai kwamba hatua ya Ujerumani kuipatia Israel msaada wa kisiasa, kifedha na kijeshi na kuondoa ufadhili kwenye shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina, UNRWA inaashiria wazi kwamba wanaratibu mauaji ya kimbari na  kwa namna yoyote ile wameshindwa kutimiza wajibu wa kufanya kila linalowezekana kuzuia mauaji ya kimbari.

Licha ya walengwa wakuu kwenye kesi hiyo kuwa ni Ujerumani, lakini inailenga pia kampeni ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza, ingawa si moja kwa moja.

Ujerumani inakana madai ya Nicaragua ikisema haijakiuka mkataba wa kuzuia mauaji ya Kimbari au sheria ya kimataifa inayohusu masuala ya  kiutu, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, sebastian Fischer, siku ya Ijumaa.