1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya ICC kumchagua mrithi wa Bensouda

12 Februari 2021

Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC wanatarajia kumchagua mwendesha mashtaka mkuu mpya kwa ajili ya mahakama hiyo, kuchukua nafasi ya kiongozi wa sasa aliyewekewa vikwazo na Marekani, Fatou Bensouda. 

https://p.dw.com/p/3pG7p
Niederlande Den Haag | ICC | Internationaler Strafgerichtshof
Picha: Everett Collection/picture alliance

Wagombea wanne kutoka Uingereza, Ireland, Italia na Uhispania wanawania kuchukua nafasi ya mwendesha mashkata anayemaliza muda wake, Fatou Bensouda, aliyeendesha uchunguzi  kuanzia mzozo wa Israel na Palestina pamoja na Afghanistan.

Vyombo vya habari vya Uingereza vimeeleza kuwa Karim Khan kutoka Uingereza anaonekana kuwa katika nafasi nzuri akiwa mbele ya Carlos Castresana kutoka Uhispania, Fergal Gaynor wa Ireland na Francesco Lo Voi wa Italia.

Uchaguzi baada ya majaribio kadhaa

Nchi wanachama za Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC zilishindwa kufikia makubaliano, licha ya majaribio kadhaa katika wiki za hivi karibuni na sasa watamchagua mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo katika uchaguzi utakaofanyika mjini New York, Marekani.

Bensouda raia wa Gambia anatarajiwa kumaliza muda wake Juni 15, baada ya kuiongoza mahakama ya ICC iliyoko mjini The Hague, Uholanzi kwa miaka tisa, hiyo ikiwa ni moja ya kazi zenye changamoto kubwa katika kazi za mahakama ya kimataifa, huku akiwa na rekodi tofauti za mafanikio.

Yeyote atakayechaguliwa kuwa mwendesha mashtaka mkuu wa tatu wa ICC tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 atakabidhiwa kesi kubwa na ngumu katika mahakama hiyo, ambao uhalali wake huwa unakosolewa kila wakati.

Niederlande Chefanklägerin beim Internationalen Strafgerichtshof in Den Haag | Fatou Bensouda
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou BensoudaPicha: Getty Images/AFP/E. Plevier

Majukumu ya mwendesha mashtaka mkuu mpya wa ICC ni pamoja na kuamua hatua zinazofuata kuhusu uchunguzi wa uhalifu wa kivita nchini Afghanistan na uchunguzi juu za mzozo wa mwaka 2014 kati ya Israel na Palestina katika Ukingo wa Gaza

Mwaka uliopita, Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump alimuwekea Bensouda vikwazo kutokana na hatua yake ya kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa nchini Afghanistan unaowahusisha pia wanajeshi wa Marekani. Hata hivyo, Marekani na Israel sio wanachama wa ICC.

Serikali ya Biden yaashiria amani

Utawala wa rais mpya wa Marekani, Joe Biden umeashiria mwelekeo wa kutozozana na mahakama ya ICC, ingawa haujaeleza iwapo utaviondoa vikwazo hivyo dhidi ya Bensouda.

ICC ni mahakama pekee ya kudumu inayoendesha kesi za uhalifu wa kivita duniani, baada ya miaka kadhaa ambapo njia pekee ya kupata haki kwa ukatili uliofanywa kwenye nchi kama Rwanda na iliyokuwa Yugoslavia ilikuwa ni mahakama tofauti.

Tangu kuanzishwa kwake na hatua ya Marekani, Urusi na China kukataa kujiunga kuwa wanachama wa ICC, mahakama hiyo imekuwa ikikosolewa kwa kuzifuatilia zaidi kesi kutoka mataifa maskini ya Afrika.

Bensouda alichukua rasmi nafasi hiyo Juni 15, mwaka 2012 kutoka kwa Luis Moreno-Ocampo raia wa Argentina.

(AFP, Reuters)