Mahakama ya Korea Kusini yakataa Rais Yoon kuachiwa huru
16 Januari 2025Hayo yamejiri siku moja tu baada ya Rais Yoon kukamatwa katika makazi yake ili kuhojiwa kuhusu madai ya uasi yanayohusishwa na tamko lake la sheria ya kijeshi mwezi uliopita.
Yoon alipelekwa kizuizini karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Seoul, baada ya kuhojiwa kwa zaidi ya saa 10 jana Jumatano katika makao makuu ya Ofisi ya Upelelezi wa Ufisadi kwa Maafisa wa Vyeo vya Juu, ambapo alitumia haki yake ya kukaa kimya.
Yoon amekataa kuhojiwa zaidi leo na maafisa wa kupambana na rushwa huku mawakili wake wakisisitiza kuwa uchunguzi huo ni kinyume cha sheria.
Wanasheria wake waliitaka Mahakama ya Wilaya ya Kati ya Seoul kumuachia huru, wakihoji uhalali wa hati ya kuzuiliwa Yoon iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Magharibi ya Seoul. Lakini Mahakama ya Wilaya ya Kati ya Seoul imekataa ombi lao.