Mahakama ya Ufilipino yamuondolea hatia Maria Ressa
18 Januari 2023Korti moja nchini Ufilipino imemuondolea hatia mshindi wa Tuzo ya Nobel Maria Ressa, ambaye pamoja na tovuti yake ya habari ya Rappler walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kukwepa kodi. Ressa ambaye aliipokea tuzo ya Nobel mwaka 2021 alikanusha mashitaka hayo mwaka 2020 akisema yalikuwa yamechochewa kisiasa.
Ukwepaji wa kodi ni moja ya tuhuma ambazo zinamuandama, nyingine zikiwa dhihaka ya kimtandao ambayo ameikatia rufaa baada ya kukutwa na hatia.
Ikiwa rufaa hiyo itaambulia patupu, mwandishi huyo mashuhuri anaweza kufungwa jela kwa karibu miaka saba. Maria Ressa alianzisha tovuti ya Rappler kupambana na taarifa za uongo na kutunza rikodi za uvunjaji wa haki za binadamu uliokuwa ukifanya na utawala wa rais wa zamani wa Ufilipino, Rodrgo Duterte, ikijikita juu ya vita vyake dhidi ya madawa ya kulevya.