1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya UN yaikataa rufaa ya Taylor

26 Septemba 2013

Mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa imetupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na kiongozi wa zamani wa Liberia, Charles Taylor.

https://p.dw.com/p/19oyY
Kiongozi wa zamani wa Liberia, Charles Taylor
Kiongozi wa zamani wa Liberia, Charles TaylorPicha: dapd

Aidha, mahakama hiyo imethibitisha kwamba kiongozi huyo aliyepatikana na hatia ya uhalifu wa kivita, ataendelea na adhabu yake ya kifungo cha miaka 50 jela.

Majaji wa mahakama hiyo maalum ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sierra Leone, leo wameikataa rufaa ya Taylor mwenye umri wa miaka 65, aliyepatikana na hatia ya makosa 11 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu, ikwemo ugaidi, mauaji, ubakaji na kuwatumia watoto katika jeshi.

Akisoma umuazi wa jopo la majaji sita wa mahakama hiyo iliyoko The Hague, Uholanzi, Jaji kiongozi wa kesi hiyo, George Gelaga King, amesema hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 50 jela, ni ya haki kutokana na makosa aliyotenda.

Hukumu ya kwanza

Taylor aliyehukumiwa mwezi Aprili mwaka 2012, amekuwa kiongozi wa kwanza wa zamani wa nchi kuhukumiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita tangu baada ya kesi ya Utawala wa Kinazi huko Nuremberg, mwaka 1946 baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Waasi wa RUF wa Sierra Leone wakiwa na wanajeshi watoto
Waasi wa RUF wa Sierra Leone wakiwa na wanajeshi watotoPicha: AP

Mahakama hiyo imemkuta Taylor na hatia ya kuwasaidia waasi wa Sierra Leone, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 11 nchini humo. Pia amepatikana na hatia ya kuandaa mashambulizi yaliyofanywa na makundi mawili ya waasi ya Sierra Leone ya Revolutionary United Front-RUF na Armed Forces Revolutionary Council-AFRC.

Kutokana na kuwasaidia waasi hao, Taylor alipewa madini ya almasi yalizopewa jina ''Almasi za Damu''. Watu wanaokadiriwa kufikia 500,000 waliuawa kabla ya kumalizika kwa vita hivyo mwaka 2002.

Elsie Keppler kutoka shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, amesema hukumu hiyo imetoa ujumbe mzito kwamba viongozi walioko madarakani wanaweza pia kushtakiwa na kuhukumiwa kutokana na uhalifu wanaoufanya.

Mawakili wake walitaka mashtaka yaangaliwe upya

Mawakili wa Taylor walitaka mashtaka dhidi ya mteja wao yaangaliwe upya, wakidai kuwa kuna makosa ya kisheria yalifanyika wakati wa kesi yake. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulitaka Taylor aongezewe adhabu yake hadi kufikia miaka 80.

Kesi hiyo ya rufaa imehudhuriwa na Memanatu Kumara, mmoja wa waathiriwa wa vita hivyo, ambaye mkono wake wa kushoto ulikatwa na kundi la RUF mwaka 1999 mjini Freetown. Akizungumza mahakamani hapo, Kumara mwenye umri wa miaka 28, amesema uamuzi huo ni sahihi na wameridhishwa nao.

Mwanamitindo Naomi Campbell
Mwanamitindo Naomi CampbellPicha: dapd

Mashahidi kadhaa walitoa ushahidi wao wakati wa kesi hiyo, akiwemo mwigizaji wa filamu Mia Farrow na mwanamitindo maarufu Naomi Campbell, ambaye alisema mwaka 1997 alipokea zawadi ya ''almasi isiyosafishwa'', wakati wa hafla ya kuchangisha fedha iliyoandaliwa na rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman