1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yaamua mzozo wa CUF

18 Machi 2019

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imekubaliana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi (CUF)

https://p.dw.com/p/3FEh7
Ringen um neue Verfassung in Tansania
Picha: DW/M.Khelef

Hatua hiyo sasa imetoa pigo kwa upande wa Maalimu Seif Sharif Hamad ambaye amekuwa katika mzozo na mwenyekiti huyo kwa muda mrefu.

Katika uamuzi wake uliosomwa leo Jaji Dk Benhajj Masoud amesema msajili wa vyama vya siasa ana mamlaka ya kutoa msimamo na ushauri alioutoa kuhusu uhalali wa Profesa Lipumba. Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania, unamaanisha kwamba Maalim Seif Sharif Hamad si Katibu Mkuu wa CUF na hiyo ni kulingana na maamuzi ya mkutano mkuu yaliyofikiwa mwishoni mwa wiki.

Muda mfupi baada ya maamuzi hayo ya mahakama kutolewa upande wa Maalimu Seif umepanga kukutana baadaye leo. Msemaji wa kambi ya Maalimu Seif, Mbarara Maharagande amesisitiza kuwa viongozi wa chama hicho wanakutana wakati huu na baadaye watatoa msimamo wao.

Upande wa upinzani hasa ule unaunda umoja wa Ukawa umesema utaendelea kuwa bega kwa bega kwa bega upande wa kambi ya Maalimu Seif wakiamini kuwa hatua hiyo waliofikia siyo mwisho wa safari.

Salimu Mwalimu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu upande wa Zanzibar ambaye pia alikuwepo mahakamani amesema chama hicho kitaendelea kuungana na kambi ya maalimu seif hadi mwisho wa safari.

Hukumu ya kesi hii ilifunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa chama cha cha cuf ambao ni wajumbe wanaomuunga mkono Maalim Seif), dhidi ya Profesa Lipumba na msajili wa vyama wakipinga uamuzi wa msajili kumtambua Profesa Lipumba kuwa bado ni mwenyekiti halali wa CUF.

Uamuzi wa mahakama umekuja siku chache baada ya wanachama wa chama hicho upande wa Profesa Lipumba kukutana kwa siku tatu jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine walimchagua kwa mara nyingine tena msomi huyo kuwa mwenyekiti.

Kuchaguliwa kwa Lipumba kulikwenda sambamba na kutakwa kwa jina la Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu mpya wa chama hicho hatua ambayo wachambuzi wa mambo wanaona kuwa huenda ikamweka katika wakati mgumu Maalimu Seif ambaye kwa muda mrefu alikuwa akitambulika kama katibu mkuu wa chama hicho.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri: Josephat Charo