1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yagoma Misri

3 Desemba 2012

Mahakama kuu ya katiba nchini Misri imesema haitasimamia mchakato wa kura ya maoni inayotarajiwa kuamua kuhusu katiba mpya

https://p.dw.com/p/16udA
Mohammed Morsi Ägypten KairoPicha: dapd

Tamko hilo linatolewa kufuatia kitendo cha waandamanaji kuizingira mahakama hiyo hivyo kuwazuia majaji kuingia ndani ya jengo la mahakama.

Mahakama hiyo imesema haiwezi kufanya kazi chini ya shinikizo na kwamba majaji hawatakutana hadi hapo watakapoona wanaweza kufanya kazi kwa uhuru.

Maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa Rais wa taifa hilo Mohammed Mursi yalisababisha kufungwa kwa mahakama hiyo hapo jana na kuacha mzozo mkubwa baina ya majaji wakuu na vongozi wa ngazi za juu wa serikali.

Mamia ya watu wanaomuunga mkono Rais Mursi wameandamana nje ya mahakama usiku kucha kuamkia siku ambayo mahakama hiyo likuwa inataka kufanya kikao kutathmini kama bunge la katiba lililoandika rasimu ya mswada ni la halali au la. Chombo hicho kinaundwa na wanasiasa wengi kutoka chama cha udugu wa Kiislamu cha rais Mursi.

Rais wa Misri Mohammed Mursi
Rais wa Misri Mohammed MursiPicha: Reuters

Uamuzi huo wa majaji unaonekana kuwa na athari kwa mpango wa Mursi wa kutaka kupitishwa wa katiba mpya kupitia kura ya maoni iliyopangwa kufanyika mwezi tarehe 15 ya Desemba. Majaji hao ndio wanaosimamia kura nchini Misri na Rais Mursi anawahitaji kutimiza malengo yale.

Licha ya mgomo huo, Makamu wa Rais Mahmoud Mekky amesema kuwa anaamini majaji watafanya kazi yao ingawa wapinzani wa Rais Mursi wamekuwa wakishinikiza majaji kugoma.

Rais Mursi mwenyewe ameendelea kutoa wito wa kuwepo kwa majadiliano ya amani akisema "Narudia nakutoa wito wa kufanyika majadiliano ya kitaifa, kuhusu wasiwasi uliopo nchini. Kwa uwazi kabisa ili kukimaliza haraka kipindi cha mpito ili kujihakikishia usalama wa demokrasia yetu mpya."

Kesi hiyo imeweka ukungu wa kisheria kwenye mkakati wa Rais Mursi wa kutafuta namna ya kujinasua kwenye mzozo wa kitaifa unaotokana na maamuzi yake ya tarehe 22 Novemba ambao uliongeza wigo wa madaraka yake na hivyo kuzusha maandamano makali ya raia yanayompinga yeye na Chama cha Udugu wa Kiislamu anachotoka.

Watu watatu wameuawa na mamia kujeruhiwa tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga mabadiliko ya utawala aliyoyafanya Rais Mursi. Wafuasi wa Mursi wapatao 200,000 wameshiriki katika maandamano kwenye Chuo Kikuu cha mjini Cairo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Maandamano mjini Cairo
Maandamano mjini CairoPicha: dapd

Wapinzani wake wako katika uwanja wa Tahrir, kituo cha mapambano kilichomtoa madarakani kiongozi wa zamani wa taifa hilo Hosni Mubarak mwaka 2011.

Profesa katika Chuo Kikuu cha Cairo Hassan Nafaa anasema kuwa Chama cha Udugu wa Kiislamu kimedhamiria kusonga mbele na mikakati yake bila kujali chochote. "Hakuna mjadala katika uamuzi huo" anasema Nafaa ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Sayansi ya Siasa chuoni hapo.

Mwandishi: Stumai George/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba