Mahmaoud Abbas aikosoa Marekani
15 Januari 2018Katika hotuba yake aliyoitoa katika baraza kuu la mamlaka ya ndani ya Palestina ambacho ni chombo chenye maamuzi Mahmoud Abbas alimkosoa Trump pamoja na sera zake kuhusiana na Palestina ikiwa ni pamoja na hatua yake ya kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israrel.
Alisema Trump anapaswa kuona aibu kutokana na madai yake kuwa wapalestina wanakataa kuzungumza kuhusiana na amani ya Masharikiya Kati na kusisitiza kuwa wapalestina wanaheshimu mazungumzo ya amani lakini pia wanayo haki ya kukataa kile ambacho hakiko katika maslahi yao.
Kauli yake inaashiria kuzorota kwa mahusiano kati ya mamlaka ya ndani ya Palestina na utawala wa rais Donald Trump.
Wapalestina wanauona uamuzi wa Trump wa kutangaza Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel kuwa umeharibu hadhi yake ya kuwa mpatanishi wa amani ya Mashariki ya Kati.
Akifafanua zaidi Abbas alisema wanatambua kuwa mji wao mkuu ni Jerusalem na kuwa hawatakubali pendekezo linalotajwa la mji wa Abu Dis kuwa mji wao mkuu wa mamlaka ya ndani ya Palestina badala ya mji wa Jerusalem kauli inayothibitisha taarifa za awali kuwa mji huo wa Abu Dis ulikuwa ukipendekezwa kutolewa kwa Wapalestina kama mbadala kwa Jerusalem.
Hadhi ya mji wa Jerusalem ni moja ya masuala muhimu na nyeti katika mgogoro uliochukua miongo kadhaa kati ya Israel na Palestina na tangazo la Trump kuhusiana na hadhi ya mji huo alilotoa Desemba 6, mwaka jana lilichochea maandamano maeneo mengi ulimwenguni.
Majadiliano ya kisiasa yatakiwa kuwa chini ya mpatanishi kimataifa
Abbas aliongeza kuwa majadiliano ya kisiasa yanapaswa kuwa chini ya mpatanishi kimataifa na siyo Marekani pekee na kuwa hakubali Marekani kuwa mpatanishi kati yao na Israel.
Ama kwa upande mwingine Abbas alisema wapalestina wamekataa hatua ya Marekani ya kusitisha malipo kwa ajili ya wapalestina waliojeruhiwa kwa karibu familia 35,000 za wapalestina waliouawa na kujeruhiwa katika mgogoro kati yake na Israel. Utawala wa Israel unasema kuwa hatua hiyo inashawishi vurugu.
Wakati huohuo utawala wa rais Donald Trump anapanga kuzuia mamilioni ya dola inazotoa kwa ajili ya wakimbizi wa kipalestina kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na kupunguza mchango wake huo katika mwaka wa kwanza kwa kiwango cha zaidi ya nusu ya fedha hizo.
Ingawa rais Donald Trump hajatoa uamuzi rasmi lakini anaonekana kutoa dola milioni 60 pekee kati ya dola milioni 125 zilizopangwa kutolewa kama fungu la kwanza kwa mashirika ya misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa. Walisema maafisa ambao hawakuwa tayari kutajwa majina kwa vile si wasemaji maalumu wa suala hilo. Maafisa hao wameongeza kuwa michango zaidi itategemea shirika linalohusika na misaada hiyo ambalo linakosolewa na Israel ikitaka lionyesha mabadiliko katika utendaji wake na pia moja ya kigezo ikiwa ni Palestina kukubali kushiriki mazungumzo ya amani.
Mwandishi: Isaac Gamba/ape/dpae
Mhariri : Gakuba, Daniel