Maisha katika eneo lililochafuliwa na mafuta
Nigeria ina hazina kubwa ya mafuta katika bara la Afrika ambayo husafirishwa duniani kote. Hata hivyo nchi hiyo haijaweza kuwaletea wakaazi wake hali bora ya maisha.
Uvuvi usiyo na tija
Wakati fulani kijiji cha Bodo katika mkoa wa Niger Delta kilitegemea uvuvi. Kuanzia mwaka 2008 na 2009, mabomba ya mafuta ya kampuni ya Shell yalianza kupita katika mji huo kusini mwa Nigeria. Watu wengi waliachana na shughuli za uvuvi. Mtu anayetaka kuishi kwa uvuvi sasa hivi, inambidi aende baharini. Na hilo linamaanisha afanye kazi kwa muda mrefu na kwa gharama kubwa.
Utegemezi wa maji
Kijiji cha Bodo kiko katika mkoa wa Niger Delta, eneo la Ogoni. Kama ilivyo hapa, maeneo mengi ya bahari katika Niger Delta yamechafuliwa na mafuta. Watu wengi katika eneo hilo wameishi kwa kutegemea maji. Na hata wakati huu, vijiji vingi vinafikika tu kwa kutumia usafiri wa majini.
Mafuta kila sehemu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) limezungumzia uvujaji wa mafuta katika maeneo kadhaa ya Ogoni. Katika ripoti yake iliyotolewa Agosti 2011, shirika hilo lilipendekeza kwamba serikali na makapuni ya mafuta yatenge kiasi cha dola za Marekani bilioni moja ili kushughulikia usafi wa mazingira. Licha ya hivyo, mafuta yanaendelea kuwepo juu ya maji hadi wakati huu.
Nigeria haina maslahi na mazingira
Chifu wa kijiji cha Bodo, Saint Emmah Pii ana hasira. "Wote tunaweza kufa hapa, tunakunywa maji yaliyochafuliwa, tunavuta hewa chafu kwa sababu ya mafuta hayo. Lakini hakuna anayeonekana kujali nje ya Bodo. Si serikali mjini Abuja wala makampubi ya mafuta wanaojali matatizo yetu", alilalamika kiongozi huyo wa kijiji.
Hakuna kinachokwenda bila dhahabu hiyo nyeusi
Tangu kugunduliwa kwa mafuta mwaka 1958, Nigeria imepanda na kuwa nchi ya sita kwa uuzaji wa mafuta duniani, linasema shirika la taifa la petroli (NNPC). Kwa hivyo serikali inaitegemea kwa kiasi kikubwa sekta ya mafuta ambayo inachangia asilimia 90 ya mapato ya nje. Kwa mantiki hiyo, mabomba kama yale yanayopita katika mkoa wa River hayana budi kuvumiliwa.
Katika kivuli cha moto wa gesi
Kila mahala katika mkoa wa Niger Delta, unakuta mioto kama huu na haijalishi kama kijiji kinachofuata kiko umbali wa kilomita 100. Katika eneo hili kuwasha gesi kulipigwa marufuku tangu mwaka 1984, lakini miaka 28 baadaye, hakuna anayejali sheria.
Matajiri lakini ni maskini
Chukwuma Samuel alionyesha hasira dhidi ya moto wenye urefu wa mita moja ambao yeye na watu wengine katika kijiji cha karibu na mji mdogo wa Egbema wanalaazimika kukubaliana nao. "Angalieni hapa, watu wana hasira", alisema huku akionyooshea kidole katika soko dogo ambako anafanyia shughuli zake. "Tunaumia hapa, tunateseka na hatujanufaika na utajiri huu wa mafuta.
Watu ndiyo wanaoamua
Makampuni ya mafuta yanapinga madai kuwa hayawajali wananchi. Shell kwa mfano inasema kupitia programu yake ya "Global Memorandum of Understanding" inatoa fedha kwa vijiji, ambapo wanachi wenyewe ndiyo wanaamua namna ya kutumia fedha hizo. Katika jimbo la Port Harcourt, fedha hizo zimetumika kukarabati hospitali ya wanawake. Wagonjwa katika hospitali hiyo walisifu mchango wa Shell.
Hakuna msaada kijijini Bodo
Kentebe Ebiaridor kutoka shirika la hifadhi ya mazingira, Environmental Rights Action (ERA) alilalamikia kukosekana kwa msaada kwa wanakijiji wa Bodo. Alisema uchafu unaoonekana ndiyo kielelezo tosha. "Watu wanahisi kutelekezwa", alisema.
Ruzuku ya mafuta kutoka serikali
Licha ya Nigeria kuwa na utajiri wa mafuta, raia wake hawapati nafuu sana katika malipo ya bidhaa hiyo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2011, lita moja ya mafuta ilikuwa inauzwa Naira 65 (euro cent 32). Mwanzoni mwa mwaka 2012 serikali ilisitisha ruzuku ya mafuta. Baada ya wiki kadhaa za maandamano, hivi sasa lita moja inauzwa Naira 97 (euro cent 50).
Ndoto ya kuwa na kiduka kidogo
Franziska Zabbey hajanufaika chochote kutokana na bei nafuu za mafuta. Anaishi kwa kilimo na hutoka Bodo kwa nadra sana. Kazi hiyo inampatia fedha kidogo sana ambayo haitoshi kukidhi mahitaji yake yote. "Kama Shell itatupa fidia kutokana na uchafuzi huu wa mafuta, nina mpango wa kufungua kiduka kidogo", anasema. Vitu vingine katika kijiji cha Bodo havina matumaini.
Mvuvi ni mvuvi tu
Ingawa maisha ya uvuvi hayawaziki tena, boti za uvuvi bado zinatunzwa vizuri. Lini zitatumika tena, hakuna anayejua. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa itachukua kati ya miaka 25 hadi 30 kulisafisha eneo la Ogoni kutokana na uchafu wa mafuta.