Majeshi ya Israel yashambulia maeneo ya Syria
9 Januari 2018Ndege za jeshi la Israel zimeshambulia eneo la Qutayfeh kaskazini mashariki mwa mji mkuu Damascus , na makombora yaliangukia karibu na maeneo ya kijeshi na kusababisha jeshi la Syria kushambulia kwa kulipiza , na kuangusha moja kati ya makombora hayo, jeshi la Syria limesema.
Israel pia ilifanya mashambulio ya makombora ya ardhini ndani ya Syria kutoka katika eneo linalokaliwa na Israel la milima ya Golan, lakini jeshi la Syria limeyashambulia makombora hayo, taarifa hiyo ilisema.
Taarifa ilisema kwamba ndege za jeshi la Israel zilishambulia tena kwa mara ya mwisho kwa maroketi manne kutoka ndani ya Israel, na kwamba mfumo wa ulinzi wa anga wa Syria ulifanikiwa kuangusha moja kati ya makombora hayo.
Jeshi la Syria limesema mfumo wa kulinda anga umefanikiwa kuangusha moja ya makombora hayo na mengine yaliangukia katika moja kati ya maeneo ya kijeshi ya syria, na kusababisha uharibifu wa mali.
Syria yashambuliwa mara kwa mara na Israel
Jeshi la Israel limekuwa likifanya mashambulizi mara kwa mara dhidi ya jeshi la Syria na washirika wake wa Lebanon, wa kundi la Washia la Hezbollah tangu mwanzo wa mzozo wa ndani wa Syria mwaka 2011.
Msemaji wa jeshi la Israel alikataa kuelezea lolote kuhusiana na taarifa iliyotolewa na Syria. Licha ya kuwa mkuu wa jeshi la Israel mwezi Agosti mwaka jana alisema kwamba wanajeshi wake waliishambulia Syria karibu mara 100, sera za Israel kwa jumla ni kutothibitisha ama kukataa operesheni kama hizo.
Israel imeapa kuizuwia Iran kutumia ardhi ya Syria kuweka vituo vyake vya kijeshi ama kupitishia silaha nzito kwenda kwa kundi la Hezbollah nchini Lebanon, kundi ambalo limekuwa likisaidia Syria katika vita vyake vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka sita sasa.
Katika taarifa yake jeshi la Syria lilirejea onyo lake la hapo kabla la kulipiza kisasi kwa mashambulizi hayo ya anga na kurudia shutuma zake za hapo kabla kwamba Israel inatumia mashambulizi hayo kusaidia makundi ya wanamgambo nchini Syria.
Israel ilikamata kilometa 1,200 za milima ya Golan kutoka Syria katika vita vya siku sita vya mwaka 1967 na baadaye kulichukua kabisa eneo hilo katika hatua ambayo haijatambuliwa na jumuiya ya kimataifa. Syria na Israel zinaendelea kuwa katika hali ya kivita, na taifa hilo la Kiyahudi lilipigana vita vikali dhidi ya Hezbollah mwaka 2006.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre
Mhariri: Yusuf Saumu