1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya kigeni yashambuliwa Kaskazini mwa Syria

16 Januari 2019

Mshambuliaji mmoja wa kujitoa mhanga amewashambulia wanajeshi wa kigeni waliokuwa wanapiga doria katika mji wa kaskazini mwa Syria wa Manbij wakati huo huo Iran yasema majeshi yake hayataondoka Syria.

https://p.dw.com/p/3BfFK
Syrien US Soldaten nahe Manbidsch
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Malla

Kulingana na shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, takriban watu saba wameuwawa na watu wengine tisa wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo.

Kundi linalojiita dola la Kiislamu limedai kuhusika na shambulio hilo. Taarifa za kijeshi na kutoka kwenye baraza la kijeshi la mji wa Manbij unaosimamiwa na wakurdi, imesema mlipuko huo ulitokea karibu na mgahawa ulio karibu na soko kuu la mji huo. Mashambulizi hayo yametokea wakati ambapo majeshi ya Marekani yameanza mchakato wa kuondoka kutoka Syria.

Wakati huo huo mkuu wa jeshi maalumu la Iran la walinzi wa mapinduzi amesema majeshi ya Iran asilani hayataondoka Syria. Mkuu huyo ametoa kauli hiyo leo sambamba na kupinga vitisho vilivyotolewa na Israel.

Majeshi ya Marekani yaliyopo nchini Syria
Majeshi ya Marekani yaliyopo nchini Syria Picha: Reuters/Handout/U.S. Army/Z. Garbarino

Shirika la habari la kihafidhina la Fars  limemnukulu Meja Jenerali Mohammed Ali Jafar akisema  wanajeshi wa Iran washauri na zana zote za kijeshi zinazohitajika kwa ajili ya kuwaimarisha wanajeshi hao zitaendelea kuwapo nchini Syria kwa lengo la kuwasaidia watu wa Syria wanaokandamizwa. Kauli ya Jenerali huyo inazingatiwa kuwa jibu kwa vitisho viliyvotolewa na waziri  Mkuu wa Israel  Benjamin Netanyahu ambaye hapo jana aliiambia Iran iyaondoe  majeshi yake kutoka Syria.   Nao wapiganaji wa kikurdi wa kikosi cha YPG wamelikataa pendekezo la Marekani juu ya kutenga ukanda wa usalama chini ya usimamizi wa majeshi ya Utruki kaskazini mwa Syria. Na Urusi  imesema ni majeshi ya Syria tu yanayopaswa kusimamia ulinzi sehemu hiyo. 

Kiongozi mwandamizi wa wapiganaji wa Kikurudi YPG amesema, baada ya kulipinga pendekezo la Marekani, wakurdi hao wako tayari kuyakubali majeshi ya Umoja wa Mataifa yawekwe kwenye sehemu inayowatenganisha wapiganaji wao na majeshi ya Uturuki, ili kuzuia mashambulio ya Uturuki na kwamba wanatarajia kufikia makubaliano na jirani yao Uturuki kuhakikisha utulivu katika eneo la mpakani.

Mapema wiki hii rais wa Uturuki Recp Tayyip Erdogan alisema kuwa majeshi ya nchi yake yatatenga ukanda wa usalama kaskazini mwa Syria baada ya rais Donald Trump kutoa wazo hilo. Rais Erdogan alisema hayo siku moja baada ya mazungumzo yake na rais Trump kwa njia ya simu.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFP/RTRE/AP

Mhariri: Josephat Charo