Makamanda wa waasi Sudan Kusini wajitenga na Machar
12 Agosti 2015Kamanda wa waasi Gathoth Gatkuoth ambaye alifutwa kazi na Riek Machar mwezi uliopita pamoja na kamanda mwingine Peter Gadet wamesema sasa watampiga vita Machar na Rais Salva Kiir.
Tayari kuna zaidi ya makundi ishirini ya waasi yanayohusika katika mzozo unaolikumba taifa hilo changa zaidi duniani la Sudan Kusini, vita ambavyo vimedumu kwa miezi kumi na tisa na kusababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwalazimu mamilioni ya wengine kuyatoroka makaazi yao.
Machar na Kiir washutumiwa
Makamanda hao wawili wa waasi wamesema Machar na Kiir wote ni ishara ya chuki, migawanyiko na uongozi ulioshindwa na kuongeza viongozi wote wawili wanawajibika kwa kuanza vita nchini humo.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vilianza mwezi Desemba mwaka 2013 wakati Kiir alipomshutumu Machar ambaye alikuwa makamu wake wa Rais kwa kupanga njama ya kumpindua madarakani na hivyo kuchochea mauaji ya kulipiza kisasi katika misingi ya kikabila.
Mazungumzo ya kutafuta amani yalianza tena katika nchi jirani ya Ethiopia wiki iliyopita huku jumuiya ya kimataifa ikishinikiza kufikiwa ufumbuzi wa mzozo huo ifikapo tarehe 17 mwezi huu.
Hata hivyo makamanda wa waasi waliojitenga na uongozi wa Machar wanamshutumu kwa kujitakia madaraka yatakayomnufaisha yeye tu na kusema hawatayatambua makubaliano yoyote yatakayoafikiwa.
Gatkuoth amesema mazungumzo yanayoendelea ni kuhusu Machar kutafuta nyadhifa wala sio ya kutafuta amani wanayoitaka na makubaliano yoyote ya amani yatakayotiwa saini hayatakuwa halali na hayataheshimiwa.
Haijabainika wazi Gatkuoth na Gadet wana kiasi gani cha vikosi vya waasi waliojitenga lakini makanda wote wawili wamekuwa na ushawishi mkubwa kwa muda mrefu katika upande wa waasi. Kutengana kwao na Machar kunatarajiwa kupunguza nguvu za Machar katika meza ya mazungumzo.
Ushawishi wa Machar huenda ukapungua
Gadet ambaye amekuwa kiongozi wa kundi la waasi sugu kwa miongo kadhaa katika jimbo la Unity, kaskazini mwa Sudan Kusini yuko katika orodha ya Umoja wa Mataifa ya watu waliowekewa vikwazo kwa kuvichochea vita nchini humo.
Kamanda huyo wa waasi anashutumiwa kwa kuidungua ndege ya Umoja wa Mataifa mwezi Agosti mwaka jana, ambapo watu watatu wote raia wa Urusi wahudumu wa ndege hiyo waliuawa.
Gadet amekanusha kuhusika katika udunguaji huo. Umoja wa Mataifa unamshutumu pia kwa kuongoza shambulizi katika mji ulio na utajiri wa mafuta wa Bentiu ambapo mamia ya watu walichinjwa.
Mwandishi: Caro Robi/afp
Mhariri:Josephat Charo