Makamanda wawili wa jeshi wakamatwa Congo
5 Septemba 2023Waziri wa mambo ya ndani Peter Kazadi amesema polisi wamewakamata kanali Mike Mikombe aliyeongoza kikosi cha ulinzi wa rais mjini Goma na Luteni Kanali Donatien Bawili aliyeongoza kikosi cha jeshi la Congo katika mji huo ambako machafuko yalitokea.
Maafisa wa jeshi na vikosi vya usalama walitumia nguvu kupita kiasi Jumatano wiki iliyopita kukandamiza maandamano dhidi ya Umoja wa Mataifa mjini Goma. Ujumbe wa serikali uliwasili Goma siku ya Jumatatu kuanza uchunguzi kwa lengo la kuwawajibisha waliohusika na waziri Kazadi amesema hawana nia ya kuficha kitu chochote akisisitiza kwamba ukweli wote utajulikana.
Maafisa wamezitaka familia za watu waliouliwa mjini Goma wajitokeze na taarifa kwa ajili ya uchunguzi.
Kazadi alisafiri kwenda Goma kufuatia ukandamizaji huo kuchunguza kilichotokea akiwa ameandamana na waziri wa ulinzi wa Congo Jean-Piere Bemba. "Tuliwahoji maafisa wote wa jeshi katika mji huo" Kazadi alisema. "Baadhi ya maafisa wa jeshi walipelekwa mara moja kwa afisi ya muendesha mashitaka ya jeshi."
"Tunawaomba umma waendelee kuwa watulivu, waiamini serikali na mfumo wetu wa sheria, ambao hivi karibuni utafikia hukumu," waziri huyo wa mambo ya ndani aliongeza kusema.
Muungano unaopigania demokrasia LUCHA umepongeza kukamatwa kwa maafisa hao wa jeshi lakini ukatoa wito meya wa Goma, gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu Kaskazini na wanajeshi wa vye vya chini waliohusika na tukio hilo pia watiwe mbaroni.
Mnamo Agosti 23 meya wa Goma alipiga marufuku maandamano yaliyopangwa na kundi la kidini la Natural Judaic and Messianic Faith Towards the Nations, unaofahamika kama Wazalendo. Wafuasi wake walipanga kuandamana dhidi ya majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na tume ya amani ya Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO.
Ujumbe huo umekabiliwa na shinikizo linalozidi ukitakiwa uondoke kutoka Congo baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miongo miwili katika nchi hiyo inayolemewa na vita.
(ap)