Makamu wa rais wa bunge la Ulaya ashtakiwa kwa rushwa
12 Desemba 2022Polisi inaendelea na uchunguzi wa tuhuma kwamba, Kaili ambaye pia ni mbunge wa ulaya kutoka chama cha kisoshalisti cha Ugiriki, alipokea rushwa kutoka kwa watu wanaofanya kazi kwa niaba ya Qatar ambaye pia ni mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia ili kushawishi mjadala wa kisera katika Umoja wa Ulaya.
Kaili ambaye amezungumza hadharani akiunga mkono mabadiliko ya sera za wafanyakazi nchini Qatar, ni miongoni mwa washukiwa wannne waliokamatwa na kuzuiliwa na polisi dhidi ya makosa hayo ya ufisadi. washukiwa wengine wawili wamechiwa huru huku wachunguzi wakipekuwa moja ya nyumba ya mbunge mwengine wa bunge la Ulaya.
Infantino: Mizozo ikome wakati wa kombe la dunia
Hata hivyo ofisi ya waendesha mashtaka wa Ubelgiji haikutoa majina ya washukiwa hao wanne waliokamatwa lakini duru kutoka shirika la habari la AFP, zilithibitisha kuwa Eva Kaili ni miongoni mwa walioshitakiwa. Taarifa kutoka ofisi hiyo imesema wanne hao wameshtakiwa kwa makosa ya kujihusisha na mashirika ya kihalifu, utakatishaji fedha, na ufisadi. Walikamatwa baada ya polisi kupekuwa nyumba zao na kukuta dola 630,000 na kukamata pia kompyuta kadhaa na simu za mkononi.
Nyumba nyengine iliyopekuliwa inaaminika kuwa ya Marc Tarabella, ambaye ni mbunge wa Ulaya pia kutoka chama cha kisoshalisti cha Uguriki na makamu mwenyekiti wa ujumbe wa bunge la Ulaya unaoshughulika na mahusiano ya rasi ya kiarabu. Tarabella bado hajashitakiwa.
Borrell asema kesi inayoendelea inatia wasiwasi mkubwa
Rais wa bunge la Ulaya Roberta Metsola alikuwepo katika operesheni ya upekuzi nyumbani kwa Tarabella, kwa sababu kulingana na katiba ya Ubelgiji, rais wa bunge la Ulaya lazima awepo iwapo mmoja ya wabunge wake katika bunge la Ulaya analengwa kufanyiwa uchunguzi wa aina yoyote.
Kwa upande wake kamishna wa masuala ya uchumi wa Ulaya Paolo Gentiloni amesema kesi hiyo inalipaka tope bunge la Ulaya na kuharibu sifa yake. Naye Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema hali inayoendelea inatia wasiwasi.
Eva Kaili kwa sasa amevuliwa majukumu yake kama makamu wa rais wa bunge la Ulaya pamoja na lile la kumuwakilisha Metsola katika eneo la Mashariki ya Kati. Anabakia kuwa mbunge wa Ulaya na bado analindwa au kuwa na kinga ya kushitakiwa dhidi ya mashtaka ya uhalifu. Lakini huenda sheria ikambana kufuatia kukutwa na begi zima lililojaa fedha nyumbani kwake.
Waendesha mashtaka wanasema watu walio katika nafasi za kimkakati ndani ya bunge la Ulaya walilipwa pesa chungu nzima ili kushawishi uamuzi wa bunge kuelekea mjadala wa kisera wa Umoja wa Ullaya bila kuinyooshea kidole moja kwa moja Qatar.
Chanzo: afp/ap