1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May atafuta uungwaji mkono katika Brexit

4 Desemba 2018

Wabunge wa Uingereza siku ya Jumanne wataanza siku tano za majadiliano kuhusu makubaliano ya Waziri Mkuu Theresa May na Umoja wa Ulaya ya kujiondoa kwenye umoja huo unaojulikana kama Brexit.

https://p.dw.com/p/39PLl
Brüssel EU Brexit Abkoomen Theresa May
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Grant

Majadiliano haya ni kuelekea kura itakayoamua mustakabali wa Uingereza na uongozi wake.

May ataufungua mjadala akisisitiza kwa mara nyengine kwamba makubaliano yake ndiyo njia ya pekee ya kujiondoa kwa amani kutoka kwenye Umoja wa Ulaya mwezi Machi mwakani.

Kulingana na dondoo kutoka kwenye hotuba yake iliyotolewa na makao makuu ya Waziri Mkuu, May, atawaambia wabunge na hapa nanukuu hotuba hiyo, "haya ndiyo makubaliano ambayo yanawapa Waingereza kile wanachotaka, watu wetu wanatutaka tuwe na makubaliano ambayo yanaiheshimu kura ya maoni na yanayotufanya tuje pamoja tena kama nchi, pasipo kujali tulivyopiga kura," mwisho wa kunukuu.

May alionya kuhusu kuyakataa makubaliano hayo 

Mpango wa Waziri Mkuu huyo wa kuweka uhusiano wa karibu na Umoja wa Ulaya umekosolewa na wanaounga mkono Brexit na kadhalika wanaopinga, jambo linalomfanya awe na wakati mgumu wa kupata idhini ya bunge katika kura itakayopigwa baada ya majadiliano hayo mnamo Desemba 11.

London House of Commons Brexit Debatte May
Mjadala unatarajiwa kuwa mkali huko Westminster Picha: picture-alliance/empics/PA Wire

May awali aliwahi kuonya kwamba kuyakataa makubaliano hayo huenda yakashuhudia Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya bila makubaliano yoyote, jambo ambalo wachumi wanaonya huenda likasababisha kudorora kwa uchumi.

Chama cha Labour ambacho kinayapinga makubaliano hayo pamoja na vyama vyote vya upinzani na ambacho kimezungumzia uwezekano wa kufanywa upya kura ya maoni, kimesema iwapo makubaliano ya May hayatoungwa mkono basi wataanzisha kura ya imani ili kuiangusha serikali ya May. Waziri Mkuu huyo ambaye amekosolewa pia na baadhi katika chama chake cha Kihafidhina huenda akakabiliwa na changamoto ya uongozi.

Wakosoaji na wanaouunga mkono Umoja wa Ulaya waungana

Lakini alipokuwa bungeni Jumatatu alishikilia kwamba makubaliano hayo yataiwezesha Uingereza kufanya biashara na hata Marekani.

"Nilizungumza na Rais Trump na nilikuwa wazi naye kwamba tunaweza kufanya biashara na Marekani kutokana na makubaliano tulioafikiana na Umoja wa Ulaya," alisema May, "na tumetambua ushirikiano ambao uko kati ya Uingereza na Marekani na tukiangalia mipango ya biashara ya siku za usoni, tumekuwa tukipiga hatua," aliongeza Waziri huyo Mkuu.

Anti Brexit Demonstration In London
Waandamanaji wanaounga mkono Umoja wa Ulaya nje ya bungePicha: picture alliance/NurPhoto/A. Pezzali

Makubaliano ya Brexit yaliyoafikiwa mwezi uliopita huko Brussels yamewaunganisha wakosoaji kutoka nyanja zote za kisiasa. Wanaoukosoa Umoja wa Ulaya wanasema ni makubaliano yatakayoifanya Uingereza kuwa taifa linaloongozwa na Ulaya huku wanaounga mkono Umoja huo wakisema Uingereza itakuwa nchi yenye kufuata upepo katika masuala ya sheria.

Mwanasheria Mkuu wa Uingereza, Geoffrey Cox amekiri makubaliano hayo "hayavutii" na "hayaridhishi" ila amesema yanahakikisha Brexit yenye amani.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo