1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yafikiwa

15 Januari 2025

Katika hatua muhimu kwenye mgogoro wa muda mrefu wa Gaza, Israel na kundi la Hamas wamefikia makubaliano ya kihistoria ya kusitisha mapigano, yaliosimamiwa na Qatar. Viongozi wa ulimwengu wamepongeza hatua hiyo.

https://p.dw.com/p/4pBPy
Ukanda wa Gaza, Deir al-Balah 2025 | Wapalestina wakisherehekea makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel
Mwanaume akipunga bendera za Palestina huku Wapalestina wakishangilia habari za makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel, mjini Deir Al-Balah, katikati mwa Ukanda wa Gaza, Januari 15, 2025.Picha: Ramadan Abed/REUTERS

Makubaliano hayo, yaliyotangazwa Jumatano jioni na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, yanajumuisha kuwachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina walioko katika magereza ya Israel.

Usitishaji huu wa vita unatarajiwa kuanza Jumapili na utaendelea kwa siku 42, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa pande hizo kusitisha mapigano tangu vita vilipoanza tena Gaza miezi 15 iliyopita.

Soma pia: Hamas yakubali rasimu ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka

"Makubaliano haya yanatoa matumaini kwa raia wa pande zote ambao wamepitia mateso makubwa,” alisema Al Thani, akihimiza pande zote kudumisha utulivu wakati wa utekelezaji wa makubaliano hayo.

Israel, Tel Aviv 2025 | Ndugu na marafiki wa waathirika wa mashambulizi ya Hamas wakitoa hisia zao kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano.
Ndugu na marafiki wa waathirika wa mashambulizi ya Hamas wakitoa hisia zao kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano.Picha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Mpango wa hatua tatu

Kwa mujibu wa Rais wa Marekani Joe Biden, usitishaji huu wa vita ni sehemu ya mpango wa hatua tatu unaolenga kufanikisha kumalizika kwa mgogoro huo kwa njia ya kudumu.

Akizungumza katika Ikulu ya White House, Biden alieleza kuwa hatua ya kwanza ni kipindi cha wiki sita cha kusitisha kabisa mapigano, kuondolewa kwa vikosi vya Israel kutoka maeneo yenye wakazi wengi Gaza, na kuachiliwa kwa mateka walioko mikononi mwa Hamas.

Katika kipindi hiki, mazungumzo yataendelea kwa lengo la kufanikisha hatua ya pili ya kumaliza vita kabisa.

"Usitishaji huu wa mapigano siyo tu muda wa kupumzika; ni hatua ya kuelekea amani ya kudumu,” alisema Biden, akisisitiza msaada wa Marekani katika kufanikisha mpango huu.

Soma pia: Mazungumzo ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas yapiga hatua kubwa

Katika awamu ya kwanza, Hamas itawaachilia huru mateka 33 wa Kiyahudi, wakiwemo wanawake, raia, watoto, wazee, na askari wanawake. Kwa upande mwingine, Israel itawaachilia huru wafungwa kadhaa  wa Kipalestina.

Qatar, Doha | Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje Mohammed bin Abdulrahman Al Thani
Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al ThaniPicha: Nathan Howard/REUTERS

Sheikh Al Thani, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika mazungumzo haya, alielezea matumaini yake kuwa usitishaji vita huu utatoa msukumo kwa mazungumzo ya amani ya baadaye.

Rais wa Israel ametoa wito kwa serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuidhinisha rasmi makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza.

Maoni ya kimataifa

Viongozi wa kimataifa wamepongeza makubaliano haya wakiwa na matumaini makubwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa vikwazo vya kiusalama na kisiasa vinavyokwamisha usambazaji wa misaada Gaza vinaondolewa.

Guterres pia ametoa wito wa kuheshimiwa kwa mipaka ya ardhi ya Palestina na juhudi za kuimarisha uongozi wa pamoja wa Palestina ambao unaweza kufanikisha amani ya kudumu.

Guterres amesisitiza juu ya umuhimu wa kuongezwa kwa misaada ya kibinadamu ili kutoa msaada wa haraka kwa wakazi wa Gaza wanaokumbwa na matatizo makubwa ya kibinadamu.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema makubaliano haya ni hatua muhimu inayofungua njia ya kumaliza vita Gaza.

Marekani, Washington 2024 | Rais Trump akihutubia baada ya mkutano na Maseneta wa chama cha Republican
Rais Mteule wa Marekani Donald Trump amesema uthabiti wake ndiyo umepelekea makubaliano kufikiwa.Picha: Annabelle Gordon/IMAGO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani alielezea kuwa makubaliano hayo ni "hatua muhimu kuelekea amani” na akasisitiza haja ya kuongeza misaada ya kibinadamu Gaza.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alitoa wito wa kuendelezwa kwa hatua zaidi kuelekea suluhisho la mataifa mawili na kuahidi msaada wa Italia katika juhudi za kuleta utulivu na kuijenga upya Gaza.

Soma pia: Biden na Netanyahu wajadili juu ya juhudi za usitishaji mapigano Gaza na kuwaachilia mateka

Naye, Rais mteule wa Marekani Donald Trump ameonyesha matumaini makubwa, akiyataja makubaliano hayo kama ushahidi wa juhudi za kidiplomasia za utawala wake.

"Makubaliano haya ya kusitisha mapigano ni MATOKEO ya ushindi wetu wa kihistoria katika uchaguzi wa Novemba,” Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

Pia alisisitiza kujitolea kwake kuendeleza makubaliano ya Abraham na kuahidi kuendelea kukuza amani kupitia nguvu.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

Shangwe na vifijo Gaza

Wakaazi wa Gaza wamelipuka kwa shangwe baada ya ripoti za kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Kwa mujibu wa mashuhuda, maelfu ya watu wenye furaha walifurika mitaani.

Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii za Palestina zinaonyesha watu wakiimba na kucheza, huku baadhi ya wanaume wakionekana wakilia kwa furaha.

Soma pia: Watoto 7 wamekufa kwa baridi kali Gaza huku makumi wakiuawa

Wakati usitishaji wa mapigano unatarajiwa kuanza, wadau wa kimataifa wameelekeza juhudi zao kuhakikisha utekelezaji wa mafanikio wa makubaliano hayo na kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ya raia wa Gaza.

Makubaliano haya yanatazamiwa kuwa mwanzo wa mabadiliko ya kudumu katika mgogoro wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.

Chanzo: Mashirika