1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha mapigano yavunjwa Syria

12 Aprili 2012

Makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria yamekiukwa leo baada ya majeshi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad kumuuwa raia mmoja wa nchi hiyo katika mji wa Hama uliopo katika eneo la kati la Syria.

https://p.dw.com/p/14cJj
Bendera ya upinzani Syria
Bendera ya upinzani SyriaPicha: Reuters

Wanaharakati wanaotetea haki za binadamu nchini Syria wameeleza kwamba mtu aliyeuwawa katika mji wa Hama alikuwa anaitwa Mahdi Ibrahim al-Ahmad na kwamba alikuwa anatafutwa na wanajeshi wa Syria. Wanajeshi hao walimuuwa kwa kumpiga risasi leo mchana baada ya al-Ahmad kukataa kusimama katika eneo la ukaguzi wa kijeshi. Kifo cha raia huyo ni cha kwanza kuripotiwa leo.

Basma Quodmani ambaye ni mmoja wa wasemaji wa baraza la taifa la Syria, ameeleza kwamba watu wengine wawili waliuwawa leo huku wengine wakikamatwa katika mikoa ya Aleppo na Daraa. "Tuna ushahidi wa picha na vidio unaoonyesha kwamba bado kuna silaha nzito katika maeneo yanayokaliwa na watu," alieleza msemaji huyo.

Erdogan ataka NATO iulinde mpaka wake

Kuna habari kwamba pametokea mlipuko wa bomu lilikuwa limetegwa katika gari. Vyombo vya habari vya Syria vimeripoti kwamba bomu hilo lililipuka mjini Aleppo na kumwua afisa mmoja wa usalama na kuwajeruhi watu wengine wasiopungua 24. Syria imeeleza kwamba bomu hilo lilitegwa na watu wanaoshukiwa kuwa magaidi. Hata hivyo hakuna uthibitisho juu ya taarifa hiyo kwani vyombo vya habari kutoka nje bado havijaruihusiwa kuingia Syria.

Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan
Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: AP

Wakati huo huo, shirika la habari la Uturuki limeripoti kwamba vikosi vya Syria vimeishambulia kwa risasi kambi ya wakimbizi iliyopo Uturuki. Risasi hizo ziliwalenga wakimbizi kutoka Syria waliokimbilia Uturuki kujiepusha na mapigano nchini mwao. Hii ni mara ya tatu ndani ya wiki moja kwa vikosi vya Syria kushambulia kambi ya wakimbizi katika nchi jirani ya Uturuki. Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema huenda nchi yake ikaiomba jumuiya ya kujihami ya NATO kulinda mpaka wake na Syria.

Kwa mujibu wa gazeti la Uturuki la Hurriyet, Erdogan alisema kwamba NATO ina jukumu la kuulinda mpaka wa Uturuki. Naye waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Ahmet Davutoglu, ameeza kuwa eneo la mpaka wa Uturuki ni sawa na eneo la mpaka la NATO. Msemaji wa jumuiya hiyo ya kujihami ameliambia shirika la habari la AFP kwamba NATO inalichukulia kwa makini jukumu lake la kuwalinda wanachama wake.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP/Reuters/RTRE

Mhariri: Saumu Yusuf