1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vyasitishwa Ukanda wa Gaza

6 Mei 2019

Maafisa katika Ukanda wa Gaza wanasema viongozi wa Palestina wamekubaliana kusitishwa kwa mapigano na Israel siku ya Jumatatu na kutilia kikomo machafuko mabaya ya siku mbili yaliyotishia kupindukia katika vita.

https://p.dw.com/p/3HyqX
Israel Gaza l Auto wurde von einer Rakete in der Nähe von Yad Mordechai im Süden Israels getroffen
Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

Kulingana na mwandishi wa shirika la habari la AFP msemaji wa Israel amekataa kutoa kauli yoyote kuhusu makubaliano hayo lakini hakujakuwa na mashambulizi yoyote ya roketi.

Maafisa kutoka kundi la Hamas na Islamic Jihad ambao hawakutaka kutambulishwa wamesema Misri ndiyo iliyosimamia makubaliano hayo ya kusitishwa mapigano. Afisa mmoja wa Misri amethibitisha hilo ingawa yeye naye hakutaka kutambulishwa. Makubaliano hayo yamekuja baada ya makabiliano makali kati ya wanamgambo wa Israel na Palestina tangu vita vya mwaka 2014.

Mashambulizi Ukanda wa Gaza yalianza Jumamosi

Jeshi la Israel mapema Jumatatu limeondoa vizuwizi vyote vilivyokuwa vimewekwa karibu na eneo la Gaza wakati wa machafuko hayo. Uongozi wa jeshi hilo umewashauri raia kuendelea na shughuli zao kama kawaida. Shule katika eneo hilo zimekubaliwa kuendelea na masomo ingawa baadhi zimefungwa kutokana na roketi mia saba zilizoishambulia Israel tangu Jumamosi.

Mashambulizi yalianza Jumamosi kutoka Gaza na Israel ikarusha makombora ya kujibu na mashambulizi hayo yakaendelea hadi jana Jumapili.

Israel Gaza l  Raketenangriffe Abwehrsystem über Netiv Haasara
Roketi mia saba zilirushwa upande wa IsraelPicha: Getty Images/AFP/J. Guez

Karibu Wapalestina 23 wakiwemo wanamgambo tisa waliuwawa Upande wa Israel watu wanne waliuwawa huku watatu kati yao wakiwa raia wa Israel. Osnat Ben Natan ni mkaazi wa Gaza.

"Watoto wangu walianza kulia, mume wangu alikuwa gorofa ya chini akimshughulikia mtu ambaye alikuwa ameshambuliwa na marisau ya kombora. Alifariki baadae mikononi mwake," alisema Osnat Ben Natan.

Israel inajiandaa kuadhimisha siku ya uhuru na pia ni mwezi wa Ramadhan kwa Waislamu wa Gaza

Rais wa Marekani Donald Trump hapo jana aliihakikishia Israel kwamba nchi yake inaiunga mkono katika mashambulizi hayo aliyoyaita ya kigaidi.

Palästina Auschreitungen im Gazastreifen
Machafuko yalianza baada ya waandamanaji wa Palestina kuuwawa IjumaaPicha: picture-alliance/ZUMA Wire/Quds Net News/H. Jedi

Mashambulizi haya yamefanyika wakati Israel ikiwa inajiandaa kuadhimisha siku yake ya uhuru baadae wiki hii huku upande wa Gaza Waislamu wakiwa wameanza kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhan hii leo.

Maafisa wa Palestina katika Ukanda wa Gaza wameituhumu Israel kwa kutochukua hatua za kutopunguza vizingiti vya kupita kwa bidhaa zake kama ilivyoahidiwa katika mikataba iliyopita.

Israel na wanamgambo wa  Palestina katika Ukanda wa Gaza wamepigana vita vitatu tangu mwaka 2008 na yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita yalikaribia kufikia hatua ya vita.

Watu milioni mbili wanaishi Gaza katika hali ngumu. Kuna uhaba wa maji ya kunywa na umeme miongoni mwa vitu vingine.