Makubaliano ya mzozo wa Ukraine yafikiwa
3 Septemba 2014Makubaliano hayo yamefikiwa wakati ambapo viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanatarajiwa kukutana kesho kuujadili mzozo wa Ukraine. Ofisi ya Rais Poroshenko, imesema kuwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine, yamefikiwa leo (03.09.2014) wakati wa mazungumzo ya simu kati ya viongozi hao wawili.
Hata hivyo, msemaji wa Rais Putin, Dmitry Peskov amekanusha taarifa za kufikiwa makubaliano hayo kwa sababu Urusi siyo sehemu ya mzozo wa Ukraine. Awali Peskov alisema mawazo ya viongozi hao kuhusu kutafuta amani ya kudumu mashariki mwa Ukraine, yanafanana. Peskov alikuwa akizungumza kwenye mji mkuu wa Mongolia, Ulanbataar, ambako Rais Putin anatarajiwa kukutana na Rais Tsakhiagiin Elbegdorj wa nchi hiyo.
Ukraine na mataifa ya Magharibi yanaishutumu Urusi kwa kupeleka wanajeshi wake pamoja na silaha mashariki mwa Ukraine, kwa ajili ya kuwasaidia waasi wanaoiunga mkono Urusi na ambao wanapambana na vikosi vya serikali.
Hata hivyo, Urusi imekanusha madai hayo. Baada ya mkutano wake na Rais Poroshenko wiki iliyopita, Rais Putin alisema majadiliano ya kusitisha mapigano hayatofanyika kwa sababu Urusi siyo sehemu ya mzozo wa Ukraine.
Waasi wataka vikosi vya serikali viondoke
Ama kwa upande mwingine, viongozi wa waasi mashariki mwa Ukraine wamesema watakubali suluhisho la kisiasa kama vikosi vya serikali vitajiondoa kwenye eneo hilo.
Waasi hao wameutwaa tena mji wenye uwanja wa ndege wa Donetsk baada ya vikosi vya serikali kuondoka. Kiongozi wa waasi wa Donetsk, Miroslav Rudenko amesema wanajeshi hao wanaondoka katika mji huo uliojitangazia kujitenga wa Jamhuri ya Watu wa Donetsk.
Hapo jana (02.09.2014), mkuu mpya wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, alisema umoja huo utaiwekea Urusi vikwazo vipya ifikapo siku ya Ijumaa. Hatua hiyo imefikiwa baada ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kudai kuwa Urusi imepeleka vifaru na wanajeshi, kusini-mashariki mwa Ukraine.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Barack Obama amesema nchi yake inathamini na kuzingatia usalama wa Estonia, ambayo ni mwanachama mwenzake wa NATO. Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa mkutano wa pamoja na Rais wa Estonia, Toomas Hendrik Ilves, kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tallinn.
Ziara ya Obama inaonyesha mshikamano na eneo la Baltic
Rais Obama anazuru Estonia katika kuonyesha mshikamano na washirika wa NATO, ambao wana hofu ya kulengwa na mashambulizi ya Urusi na atakutana pia na viongozi wa Latvia na Lithuania.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Urmas Paet anasema Urusi inajihusisha moja kwa moja na uvamizi na hadi sasa hakuna jaribio lolote la kisiasa wala kidiplomasia kuutatua mzozo huo.
Amesema ni muhimu kwa NATO kujadiliana kwa kina hapo kesho na keshokutwa kuhusu hali ya Ukraine na pia iwe tayari kufanya maamuzi jinsi ya kuisaidia ukraine na nini cha kufanya ili kuzuia uvamizi.
Hayo yanajiri wakati ambapo mkutano wa kilele wa NATO kuujadili mzozo wa Ukraine ukitarajiwa kufanyika Wales, hapo kesho.
Mkutano wa NATO unatarajiwa kuidhinisha hatua za kuchukua kukabiliana na uchokozi unaofanywa na Urusi dhidi ya Ukraine. Aidha, NATO inazingatia kuongeza uwepo wake wa kijeshi mashariki mwa Ulaya.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE,DPAE,AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga