Makubaliano ya serikali mpya ya muungano Groko Magazetini
13 Machi 2018Tunaanzia Syria ambako miaka takriban saba tangu vita viliporipuka, hakuna ishara ya kupatikana amani. Zaidi ya watu 350.000 wanasemekana wamepoteza maisha yao na mamilioni wameyapa kisogo maskani yao. Jumuia ya kimataifa inalaumiwa kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo na sio tu nchini Syria. Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: "Wenye kubeba jukumu la kumomonyoka mwongozo wa kimataifa ni wengi. Urusi ndio ya mwanzo. Lakini na mataifa mengine manne ya kudumu ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa; Marekani, China, Ufaransa na Uingereza nayo pia yanafaa kulaumiwa. Hawafanyi vya kutosha kuhakikisha muongozo wa kimataifa unafuatwa. Mataifa matano yenye kura ya turufu, yamejitwikwa wenyewe jukumu hilo Umoja wa mataifa ulipoundwa. Na kwa namna hiiyo mataifa hayo yanabeba jukumu kubwa na la aina pekee mbele ya Umoja wa mataifa. Hawastahiki lakini kubeba jukumu hilo. Wanaoathirika ni wahanga wasiokuwa na idadi wa visa vya ukandamizaji, matumizi ya nguvu katika kila pembe ya dunia, sio tu nchini Syria."
Uingereza yavuta wakati katika utaratibu wa Brexit
Kitandawili cha kujitenga Uingereza na Umoja wa Ulaya, Brexit bado hakijafumbuliwa. Hasara ya aina gani itapatikana na nani wa kugharimia ndio suala analojiuliza mhariri wa gazeti la "Sudwest Presse" anaeandika: "Mbaya zaidi ni ile hali kwamba mpaka sasa, utaratibu kamili wa kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, bado haujafafanuliwa. Kipindi cha mpito cha mwaka mmoja ndicho makampuni yalichopendekeza yapatiwe. Lakini mpaka sasa si mengi yaliyofanyika kwasababu, waengereza wanaona bora kuziweka kando mada mfano kanuni za raia wa nchi za Umoja wa ulaya au mustakbali wa jimbo la Ireland ya kaskazini, na badala yake kutanguliza mbele ndoto kuhusu makubaliano ya siku za mbele ya kibiashara. Kila siku inayopita ni mtihani kwa makampuni ya wastani tena ya pande zote mbili. Wakati unawaponyoka."
Mhula wa nne wa kansela Merkel utaanza kesho
Makubaliano ya kuundwa serikali mpya ya muungano kati ya CDU/CSU na SPD yametiwa saini na viongozi wa vyama hivyo vitatu jana mjini Berlin. Kuna wanaoyatia ila makubaliano hayo. Hata hivyo gazeti la Reutlinger General-Anzeiger linayataja makubaliano hayo kuwa ni fursa ya maana. Gazeti linaendelea kuandika: "Hata kama wananchi wengi wameshaanza kuyatia ila wakidai eti hayatotekelezwa, lakini makubaliano haya mepya ya GROKO ni fursa njema inayoweza kuinua siasa ya ndani na ya nje ya Ujerumani."
Mkataba wa kuunda serikali mpya ni fursa njema kwa Ujerumani
Gazeti la Mannheimer Morgen linakumbusha wajibu wa Groko na kuandika: "Wajibu wa serikali mpya ya muungano wa vyama vikuu GroKo ni hukakikisha maamuzi ya kisiasa yanatekelezwa kwa namna ambayo wahusika wanatambua kwamba hali zao za maisha zinaimarika. Kwa namna hiyo na vyama vikuu pia vitaimarika ."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Mohamed Abdul Rahman