Makundi ya mgambo yatishia amani Uganda
2 Machi 2016Wapigakura nchini Uganda watakwenda vituoni mwezi Februari kumchagua rais pamoja na wabunge, uchaguzi ambao matokeo yake yanajulikana. Rais wa sasa Yoweri Museveni, alieko madarakani kwa karibu miaka 30 sasa, anaamini kuwa nchi yake bado inamhitaji ili kuiletea maedeleo ya kiuchumi na tayari ametangaza kugombea tena wadhifa huo. Upande wa upinzani yuko Kizza Besigye ambaye tangu mwaka 2001 amekuwa mpinzani mkuu wa Museveni.
Lakini hali ni ya wasiwasi kuelekea uchaguzi huo, na hofu inazidi kutanda kuhusu uwezekano wa kutokea vurugu katika uchaguzi huo. Katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa kwamba chama tawala - NRM kimekuwa kikitoa mafunzo ya mgambo kwa kundi la vijana, mhusika mkuu wa kundi akiwa mshauri wa rais na afisa wa zamani wa jeshi Meja Roland Kakooza Mutale, ambaye anaelezwa kuwa kiongozi wa kundi la vijana wapatao 500, walioendesha vurugu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2006.
NRM yamkana Kakooza Mutale
Chama tawala cha NRM kimekanusha kuhusika kwa vyovyote vile na harakati za Mutale. Katika mahojiano na DW, waziri wa mawasiliano wa Uganda Jim Muhwezi, alisema sheria laazima izingatiwe, na kwamba yeyote anaekwenda kinyume atawajibishwa kisheria, na kuongeza kuwa vipo vyombo vya dola vya kutosha kushughulikia masuala ya usalama wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu.
Baada ya picha za kambi ya mafunzo ya Kakooza Mutale kuonyeshwa kwenye televisheni nchini Uganda, wanasiasa wa upinzani walionyesha ghadhabu. Lakini mwanasiasa wa chama cha upinzani cha Democratic DP, Erias Lukwago ambaye pia ni meya wa jiji la Kampala, hakutaka mambo yaishie hapo tu. Naye alianzisha kundi lake la vijana alillolitaja kama kundi lao la kujihami na kuiambia DW kuwa maisha yao yalikuwa hatarini.
Matukio hayo yamezusha hasira miongoni mwa raia wa Uganda, na hofu inazidi kuongezeka kwamba makundi hayo huenda yakaitumbukiza nchi katika machafuko. Kutokana na hali hiyo, polisi imewaita Mutale na Lukwago kuwahoji na msemaji wa jeshi la polisi Fred Enanga alitahadharisha kuwa yeyote mwenye mpango wa kuunda makundi kama hayo atawajibishwa.
Zipo fununu pia kuwa waziri mkuu wa zamani na mshirika wa rais wa rais Yoweri Museveni Amama Mbabazi, anapanga kuanzisha kundi lake la mgambo. Mbabazi alifukuzwa kutoka chama cha NRM mwishoni mwa mwezi Julai kufuatia mzozo wa ndani kuhusu uteuzi wa mgombea urais, na sasa anataka kusimama kama mgombea binafsi. Mwanasheria huyo ni miongoni mwa wanasiasa wenye mvuto nchini Uganda, na wangalizi wanasema anaweza kutoa upinzani mkali kwa rais Museveni katika uchaguzi wa Februari.
Viongozi wa dini watahadharisha
Wakati huo, baraza la viongozi wa dini nchini Uganda limejiunga pia na mjadala huo. Wajumbe wa baraza hilo wamewatolea wito wanasiasa kuzuwia kuibuka kwa makundi ya wanamgambo. Mufti Mkuu Sheikh Shaban Mubajje aliwaonya katika taarifa ya wawakilishi wa baraza hilo kuwa makundi hayo ni hatari kwa mustakabali wa taifa, na kulitaka jeshi la polisi kuwachukulia hatua kali wote wanaohusika na uanzishwaji wa makundi hayo.
Uundwaji wa makundi ya vurugu kuelekea uchaguzi nchini Uganda ni utamaduni unaozidi kukita mizizi. Mwaka 2011, polisi ilisema kulikwepo na makundi saba ya wanamgambo yaliyojipa yenyewe jukumu la kutoa ulinzi, lakini polisi ilifanikiwa kuyavunja makundi hayo kabla ya uchaguzi. Inahofiwa kuwa vurugu zinaweza kutokea, ikiwa mamlaka hazitachukuwa hatua za haraka kushughulikia tatizo hilo.
Mwandishi: Alex Gitta
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Saumu Yusuf