Mali yawakamata maafisa 4 wa kampuni ya madini ya Canada
27 Novemba 2024Utawala wa kijeshi wa taifa hilo la Afrika Magharibi linaendelea kuwakamata wafanyakazi ili kuzishinikiza kampuni katika sekta yake muhimu ya madini kulipa mamilioni katika kodi za ziada. Kampuni ya Barrick Gold imethibitisha katika taarifa kuwa wafanyakazi wake katika mgodi wa Loulo-Gounkoto wamefunguliwa mashitaka na wasubiri kesi yao baada ya kukamatwa Jumatatu jioni. Kampuni hiyo imesema inapinga mashitaka hayo lakini haikusema ni mashitaka gani. Maafisa wa Mali walikataa kuzungumzia ukamataji huo. Mapema mwezi huu, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Australia ya Resolute Mining na wafanyakazi wawili walikamatwa katika mji mkuu wa Mali, Bamako. Waliachiwa huru baada ya kampuni hiyo kulipa dola milioni 80 kwa mamlaka za Mali ili kutatua mzozo wa kodi na kuahidi kulipa dola milioni 80 nyingine katika miezi ijayo.