Malori ya misaada kutoka Misri yaanza kuingia Gaza
26 Mei 2024Shirika la habari la Misri la Al-Qahera limeripoti kuwa jumla ya malori 200 yameondoka kutoka upande wa Misri wa kivuko cha Rafah ambacho kimefungwa tangu mapema mwezi Mei baada ya jeshi la Israel kuchukua udhibiti wa eneo hilo upande wa Palestina.
Al-Qahera hata hivyo halikuweka wazi idadi ya malori yaliyofanikiwa kufanyiwa ukaguzi na kuingia Gaza, japo limeripoti kuwa tayari malori manne ya kubeba mafuta yameingia Gaza na sasa yanaelekea hospitali.
Soma pia: Mapigano yanaendelea katika mji wa kusini mwa Gaza Rafah
Mkuu wa shirika la hilali nyekundu la Misri Khaled Zayed katika eneo la Al-Arish ambapo misaada mingi huwasili, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa malori yaliyosalia yanatarajiwa kuvuka na kuingia Gaza leo.
Misaada yote kutoka Misri kwanza hukaguliwa na mamlaka ya Israel na kusambazwa kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa.