Malori yachomwa moto katika mashambulizi ya Afrika Kusini
12 Julai 2023Hii leo washambuliaji wasiofahamika waliyatia moto malori manne katika jimbo la kaskazini mashariki la Mpumalanga ikiwa ni tukio la hii karibuni kabisa la mfululizo wa matukio hayo yaliyozusha wasiwasi miongoni mwa kampuni za usafirishaji.
Mashambulizi hayo yalianza siku ya Jumapili, wakati wa kumbukumbu ya miaka miwili tangu kuzuka machafuko makubwa ya Julai mwaka 2021 yaliyoanza kwa kuchomwa moto malori. Hujuma hizo zilisambaa na kugeuka machafuko makubwa kuhawi kushuhudiwa nchini humo tangu kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi mwaka 1994.
Waziri anayeshughulikia idara ya Polisi Bheki Cele amewaambia waandishi habari mjini Pretoria kuwa wanafahamu uhalifu huo ni wa kupangwa na taarifa za kijasusi zinaashairia yana mafungamano na uhasama wa kibiashara. Kwenye matukio hayo madereva walilazimishwa na watu wenye silaha kuyatekeleza magari yao ambao baadaye waliyateketeza kwa moto.