Malumbano kati ya Uturuki na wasahirika wa NATO
14 Machi 2017
Tunaanza na mzozo unaozidi makali kati ya Uturuki na washirika wake wa jumuia ya kujihami ya NATO. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wana maoni makali dhidi ya msimamo shupavu wa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Gazeti la Wetzlarer Neue Zeitung linaandika: "Kwamba zamani Ulaya na Marekani zilipendelea zaidi kuwa na uhusiano mzuri na Uturuki, chanzo cha hali hiyo ilikuwa nafasi ya mshirika huyo wa NATO katika mzozo kati ya kambi za mashariki na Magharibi, mzozo wa mashariki ya kati na pia mzozo wa wakimbizi. Lakini kutokana na hali namna ilivyo hivi sasa, nchi za magharibi zinabidi zijitafutie haraka mshirika mwengine wa kikanda-labda Iran inayoweza kuangaliwa kama nguzo ya utulivu na maendeleo katika kanda hiyo. Siasa ya maana ni ile yenye kufuata msingi wa ushirikiano na kuheshimiana. Makosa hapo hayapo upande wa Ujerumani wala Uholanzi-yanakutikana upande wa Uturuki: "
NATO, mdhamini wa amani
Katika wakati ambapo gazeti la Trierischer Volksfreund linakosoa msimamo shupavu wa rais Erdogan, lile la Stuttgarter Zeitung linaisifu jumuia ya kujihami ya NATO kuwa mdhamini wa usalama. Gazeti linaendelea kuandika: "Waziri mkuu wa Uholanzi anaejikuta katika kampeni za uchaguzi nchini mwake, hajababaishwa na uchokozi wa Recep Tayyip Erdogan. Lakini rais huyo wa Uturuki ndie aliyeudhika na kutoa matamshi makali kwa namna ambayo mtu angeweza kuashiria tangazo la vita ni suala la wakati tuu. Hata kama mengi ni vitisho vitupu na hakuna haja ya kuhofiwa risasi kufyetuliwa, hata hivyo ni muhimu kwamba jumuia ya kujihami ya NATO imetoa wito wa subira na kupunguza mivutano. Hata kama Erdogan anaonyesha kumnyemelea zaidi rais wa Urusi Vladimir Putin, lakini jumuia ya NATO ni na itaendelea kuwa mdhamini wa usalama wa nchi iliyozungukwa na maeneo ya mizozo."
Ziara iliyopangwa ya kansela Merkel Washington
Kansela Angela Merkel alikuwa afike ziarani Marekani leo, lakini ziara hiyo imeakhirishwa kutokana na hali mbaya ya hewa inaopiga Washington. Gazeti la Mittelbayerische Zeitung linaandika kuhusu changamoto zinazomkabili kansela Merkel: "Angela Merkel ametambua zamani kwamba Trump analenga kuidhoofisha Ujerumani na Umoja wa Ulaya pia. Ili kulifikia lengo hilo, rais Trump anatumia hoja za wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Uholanzi, Ufaransa na Uingereza na kujaribu wakati huo huo kupalilia hisia za kale dhidi ya Ulaya ya kati. Jukumu la Merkel mjini Washington litakuwa kuzuwia balaa. Na ili kulifikia lengo hilo anahitaji mwongozo. Kipa umbele hapo kama wasemavyo wanadiplomasia, ni kuzungumzia masuala ya masilahi ya pamoja na kuyafafanua ni yepi. Kwa kuzingatia uhusiano wa dhati uliodumu zaidi ya miaka 70 kati ya washirika wa jumuia ya NATO, basi mtu anaweza kusema masilahi yako mengi tu.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanadsprese
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman