1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Mamia waandamana kukamatwa kwa Imran Khan wa Pakistan

9 Mei 2023

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Imarn Khan amekamatwa mapema mjini Islamabad muda mfupi baada ya kutoka mahakamani alikofikishwa kusikiliza kesi yenye mashtaka chungunzima ya rushwa na ufisadi.

https://p.dw.com/p/4R6cC
Pakistan I Wafuasi wa Imran Khan wakipambana na polisi
Wafuasi wa waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan wakiandamana kufuatia kukamatwa kwa kiongozi huyo Picha: Akhtar Soomro/REUTERS

Kulingana na taarifa za mashirika mawili ya habari lile la Associated Press na AFP, Khan alikamatwa nje ya mahakama kwenye Mji Mkuu wa Pakistan, Islamabad na maafisa wa taasisi ya kushughulikia uwajibikaji wa  viongozi wa umma.

Mawakili na mashuhuda wamesema maafisa hao walimvizia kiongozi huyo, wakamkamata kwa nguvu, wakamshambulia na kisha wakamburura hadi kwenye gari yao na kuondoka naye kusikojulikana.

Aquil Niazi ni mmoja ya mawakili wa Khan "Leo (Khan) alipokwenda kuchukuliwa alama za vidole, walimkamata kwenye viunga vya mahakama. Wakampiga kwa fimbo kichwani halafu wakampulizia kitu ambacho nusra kimfanye apoteze fahamu. Nadhani walimpulizia kitu. Baadaye wakamwingiza kwenye gari"

Afisa mwandamizi wa chama cha Khan cha Tehreek-e-Insaf, Fawad Chaudhry ametoa simulizi sawa na hiyo na kutumia mahojiano yake na kituo kimoja cha televisheni kulaani kukamatwa kwa kiongozi huyo wa zamani wa Pakistan. Amelifafanisha tukio na utekaji nyara.

Mamlaka zasema Khan amekamatwa kutokana na tuhuma za ufisadi 

Pakistan I Wafuasi wa Imran Khan
Vurugu zimesababisha watu kadhaa kujeruhiwa.Picha: Asif Hassan/AFP

Muda mfupi baada ya kukamatwa kwake chama chake kililalamika mbele ya mahakama, na chombo hicho kiliitaka polisi kutoa maelezo ya sababu za kukamatwakwa waziri huyo mkuu wa zamani.

Kulingana na polisi na maafisa wa taasisi za serikali, mwanasiasa huyo amepelekwa kwenye mji wa Rawlpindi kwa mahojiano na kufanyiwa vipimo vya matibabu. Hata hivyo waziri mambo ya ndani wa Pakistan alisema baadaye Khan amekamatwa kuhusiana na tuhuma za kujipatia sehemu kubwaardhi kwa njia za kifisadi.

Amesema akiwa madarakani Khan alipatiwa ardhi hiyo na tajiri mmoja kwa makubaliano ya kumpatia bwenyenye huyo maslahi fulani fulani ndani ya serikali yanayokadiriwa kufikia kiasi rupia bilioni 7 za Pakistan.

Madai hayo mapya ni sehemu ya mengine chungunzima ambayo Khan anakabiliwa nayo tangu alipondolewa madarakani Aprili mwaka uliopita baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.

Kimsingi hii leo alifikishwa mahakama kujibu mkururo wa kesi za ufisadi na tuhuma za ugaidi ambazo zote anakanusha akisema zimechochewa kisiasa.

Maandamano yatikisa miji ya Pakistan kufuatia kukamatwa kwa Khan

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan Picha: imago images/Russian Look

Saa baada ya kusambaa taarifa za kukamatwa kwake mamia ya wafuasi wake waliteremka mitaani  kwenye miji kadhaa ya Pakistan kulaani kisa hicho. Polisi ilipambana na wafuasi wa Khan kwa kutumia maji ya kuwasha na mabomu ya machozi kwenye miji ya Karachi, Lahore, Islamabad, Rawalpindi na Peshawar.

Hadi sasa taarifa zinasema watu kumi ikiwemo polisi sita wamejeruhiwa kwenye mji mwingine wa Quetta kwenye makabilianao kati ya polisi na wafuasi wa Khan.

Kukamatwa kwa mwanasiasa huyo kunatishia kuitumbukiza Pakistan kwenye mzozo mkubwa, taifa ambalo tayari lina matatizo lukuki tangu ya kiuchumi na kisiasa.

Kuna wasiwasi kuwa kushikiliwa kwako kunaweza kuzusha vurugu za kutisha ikitiliwa maanani kuwa bado anao ushawishi mkubwa ndani ya taifa hilo lenye nguvu za nyuklia.