1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia waandamana kupinga kufungwa wapinzani Tunisia

10 Aprili 2023

Mamia ya watu waliandamana katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis, siku ya Jumapili (Aprili 9) wakitaka kuachiliwa huru kwa wapinzani 20 wa Rais Kais Saied waliokamatwa tangu mwezi Februari.

https://p.dw.com/p/4Pryv
Protest Tunesien
Picha: Yassine Gaidi/AA/picture alliance

Takribani waandamanaji 300 kutoka vyama vya upinzani walipeperusha bendera za Tunisia na kubeba mabango yenye picha za wafungwa kwenye maandamano yalixoandaliwa na muungano mkuu wa upinzani, National Salvation Front.

Tangu mwezi Februari mamlaka katika taifa hilo la Afrika Kaskazini zimewakamata zaidi ya wapinzani 20 wa kisiasa na watu binafsi.

Soma zaidi: Rais wa Tunisia akataa masharti ya IMF kuhusu mkopo
Wafuasi wa Rais Saied waandamana Tunisia

Miongoni mwa waliokamatwa ni wanasiasa wa upinzani, mawaziri wa zamani, wafanyabiasha, wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi pamoja na mmiliki wa kituo mashuhuri cha redio nchini humo, Mosaique FM, hatua ambayo imekosolewa vikali na watetezi wa haki za binaadamu kimataifa.

Rais Saied ambaye amechukua karibu mamlaka yote tangu alipolisimamisha bunge na kuifuta serikali, anadai waliokamatwa walikuwa "magaidi" waliohusika katika "njama dhidi ya usalama wa taifa".

Wapinzani wanamshutumu kwa kuirejesha nchi hiyo iliyokuwa ya kidemokrasia katika utawala wa kiimla.