1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia wafa kwa baridi Urusi

27 Desemba 2012

Idadi ya waliofariki kutokana na baridi kali nchini Urusi imefikia 128 katika siku kumi zilizopita huku taarifa zaidi zikisema watu wengine 900 wamepelekwa hospitali kutibiwa kwa kuathiriwa na baridi hiyo.

https://p.dw.com/p/179OL
Baridi kali Urusi.
Baridi kali Urusi.Picha: Reuters

Shirika la habari la Interfax limeripoti kuwa kiwango cha hali yajoto kimeshuka na kufikia nyuzi joto 30 chini ya sifuri katika kipimi cha Celcius mjini Moscow huku Mashariki mwa Siberia hali imefikia nyuzi joto 60 chini ya sifuri.

Shirika la habari la Interfax limemnukuu mmoja wa wataalamu wa afya akisema kuwa ''Tangu kuanza kwa baridi, watu 123 wamefariki kutokana na baridi kali na kupata ugonjwa wa kuganda kwa tishu'', lilisema shirika hilo la habari.

Chanzo hicho kimesema kwamba zaidi ya watu mia nane wamelazimika kupelekwa hospitali kutokana na joto mwilini kushuka na kupata ugonjwa wa kuganda kwa tishu, wakiwemo watu 123 katika kipindi cha saa 24 , miongoni mwa wote wapo watoto 14. Tangu kuanza kwa msimu wa baridi jumla ya watu 1,745 wameathirika vibaya na baridi kali.

Hali ya dharura yatangazwa

Televisheni ya taifa hapo jana ilieleza kuwa hali ilikuwa mbaya katika kijiji cha Khovu Aksy huko Tyva, moja ya eneo maskini nchini Urusi kusini mwa Siberia. Hali ya dharura ilitangazwa baada ya kituo cha umeme kushindwa kufanya kazi kutokana na hali joto kufikia nyuzi joto 40 chini ya sifuri na kuathiri wakaazi wapatao elfu nne.

Mbwa akipita mbele ya kifaru kilichofunikwa kwa barafu nchini Urusi.
Mbwa akipita mbele ya kifaru kilichofunikwa kwa barafu nchini Urusi.Picha: Reuters

Mmoja wa wakaazi wa eneo hilo wakati akizungumza na kituo cha Vesti-24 alisema na hapa namnukuu ''Hakuna kitu, hata maji, tunayeyuka na theluji na joto nyumbani ni chini ya sifuri'' alimalizia mkazi huyo. Baadhi ya wakazi wakiwemo watoto wameondolewa kwa helikopita na kupelekwa katika jimbo la Kyzyl.

Katika nchi jirani ya Ukraine hali kama hiyo ya baridi kali imeua jumla ya watu 83 hadi kufikia wiki iliyopita ambapo wizara ya afya imesema kuwa takwimu mpya zitatolewa siku ya Ijumaa.

Marekani nako hali mbaya

Nchini Marekani kimbunga kikali cha baridi kimelazimu kuahirishwa kwa safari za ndege zipatazo 200 hii leo, wakati ambapo theluji nzito na upepo mkali ulipiga eneo la kaskazini mashariki mwa Marekani.

Baridi imefikia -8 nchini Urusi.
Baridi imefikia -8 nchini Urusi.Picha: Reuters

Mamlaka ya hali ya hewa imesema theluji ya kiwango cha inchi 12 hadi 18 imeanguka katika mji wa New England huku kimbunga kikiendelea katika eneo la Michigan. Watu wapatao watano wameripotiwa kupoteza maisha katika ajali za barabarani kutokana na hali mbaya ya hewa.

Mwandishi:Sylvia Mwehozi/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Josephat Charo