1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa Kusini mwa Afrika

Angela Mdungu
16 Oktoba 2024

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP limesema mamilioni ya watu Kusini mwa Afrika wanakabiliwa na njaa ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa iliyotokana na ukame mkali.

https://p.dw.com/p/4lrX4
Ukame Tigray, Ethiopia
Ukame katika moja ya nchi za Kusini mwa Jangwa la SaharaPicha: Million Haileselassie Brhane/DW

Hali hiyo inayotishia kusababisha mgogoro wa kiutu imeshawaathiri watu wasiopungua milioni 27 katika kanda hiyo. Nchi tano zikiwemo Lesotho Malawi, Zambia na Zimbabwe zimeshatangaza hali ya hatari katika miezi iliyopita wakati ukame ukiyaangamiza mazao na mifugo. Shirika la Mpango wa chakula duniani WFP limeeleza katika mkutano wake wa na wanahabari mjini Geneva Jumanne kuwa Angola na Msumbiji pia zimeathiriwa vibaya na hali hiyo.

Soma zaidi: El Nino, sio mabadiliko ya tabianchi, chanzo cha ukame

Akizungumza katika mkutano huo Afisa mawasiliano wa kanda katika shirika hilo Tomson Phiri amesema ukame wa  kihistoria na mgogoro mbaya wa njaa umesababisha athari kwa zaidi ya watu milioni 27 katika kanda nzima na watoto milioni 21 wana utapiamlo.

Phiri ameongeza kuwa kwa jamii nyingi huu ni mgogoro mbaya zaidi katika kipindi cha miongo kadhaa na kuwa mwezi Oktoba kanda ya Kusini mwa Afrika inapitia msimu mbaya katika mavuno. Amebainisha kwamba kila mwezi unatarajiwa kuwa mbaya zaidi kuliko uliopita, hadi mavuno ya mwaka ujao katika miezi ya Machi na Aprili.

WFP linaendelea kugawa chakula na kuendesha miradi ya kutoa misaada lakini hadi sasa limepokea humuthi pekee kati ya kiasi cha dola za Kimarekani milioni 369 zinazohitajika kukabiliana na njaa. Msaada wa haraka unatakiwa ili kuzuia ukame katika kanda hiyo ya Kusini mwa Afrika usiwe janga kamili la kiutu.

Elnino yatajwa kuwa chanzo cha ukame na hali mbaya ya njaa

Ukame uliosababisha njaa kali umechochewa na kujirudia mara kwa mara kwa na Elnino, aina ya hali ya hewa inayosababisha kukauka kwa badhi ya maeneo na mvua kubwa kupindukia katika sehemu nyingine.

Zaidi ya watu milioni 27 wanakabiliwa na njaa barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara
Watoto milioni 21 Kusini mwa Jangwa la Sahara wana utapiamloPicha: Patricia Simon/AP Photo/picture alliance

Bei za vyakula katika kanda hiyo zimepanda kwa haraka katika sehemu nyingi zilizoathiriwa na ukame, hali inayopelekea ugumu zaidi wa maisha.

Soma zaidi: WFP inahitaji dola milioni 400 kuwalisha mamilioni ya watu wanaohitaji msaada Barani Afrika

Kutokana na ukame, Zambia imeshindwa kuzalisha umeme na imekuwa ikipitia mgao kwa saa kadhaa na wakati mwingine siku kadhaa. Hii ni kwasababu taifa hilo linategemea umeme unaozalishwa katika mtambo ulio kwenye bwawa kubwa la Kariba. Zimbabwe inayotegemea pia bwawa hilo nayo inakabiliwa na tatizo la kukatika kwa umeme.

Kufuatia njaa kali, mamlaka za Namibia na Zimbabwe zimekubali kuwauwa wanyamapori wakiwemo tembo ili kuwapa nyama watu wanaokabiliwa na njaa

Wanasayansi wanasema kuwa, eneo la Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara ni moja ya maeneo yaliyo hatarini zaidi kukumbwa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na kufanya shughuli za kilimo kinachotegemea mvua, na maliasili.