Mamlaka za Uganda zatakiwa kumwachia huru Bwayo
5 Machi 2020Kamati hiyo imetaka pia mwandishi huyo arejeshewe vifaa vyake vya kazi bila kuharibiwa na aruhusiwe kuendelea na shughuli zake bila vitisho.
Bwayo alikamatwa katika mji mkuu Kampala tarehe 24 mwezi Februari wakati akitengeneza filamu fupi aliyoagizwa na kampuni ya Southern films yenye makao yake nchini Uingereza. Filamu hiyo ni kuhusu mwanasiasa wa upinzani na mwanamuziki maarufu Robert Kyagulani anayejulikana pia kama Bobbi Wine.
Kwa mujibu wa chama cha waandishi wa kigeni cha Uganda na kauli ya kundi la mtandao wa kutetea haki za binadamu kwa waandishi Bwayo aliachiliwa tarehe 26 mwezi huohuo wa pili kwa dhamana. Vyanzo hivyo vinasema pia kwamba polisi walivificha vifaa vyake. Jana alipandishwa kizimbani akituhumiwa kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria sambamba na watu wengine 8 na kisha kuwekwa katika gereza la Luzira.
Dhamana yatajwa kukwamisha Bwayo kuachiliwa huru
Mwanasheria wa Bwayo Caleb Alaka alikiambia chama cha kuwalinda waandishi wa habari cha CPJ kuwa mwandishi huyo aliwekwa gerezani baada ya mwendesha mashtaka wa serikali na hakimu kusema kuwa wanahitaji muda zaidi kujibu ombi lake la dhamana.
Mwakilishi wa chama hicho katika nchi zilizo katika jangwa la Sahara Muthoki Mumo amesema, kimsingi mwandishi huyo hakupaswa kukamatwa, na kitendo cha kuwekwa jela kinaonesha namna ambavyo serikali ya Uganda inaweza kufanya lolote ili kuzuia watu kuripoti kuhusu upinzani hasa Bobi Wine.
Muthoki amesema mamlaka za Uganda zinapaswa kumfutia mashtaka Bwayo mara moja na kumruhusu kuendelea kutengeneza makala yake bila kumuingilia. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters mahakama na serikali ya Uganda hazikupatikana kwa haraka kutoa neno lolote kuhusiana na kesi hiyo.
Katika miaka miwili iliyopita, Chama cha kuwalinda waandishi wa habari CPJ kimerekodi matukio kadhaa ambapo wanausalama na maafisa wa serikali wamekuwa wakiwanyanyasa, na kuingilia kazi za na waandishi wanaoandika kuhusu upinzani hasa Bobi Wine.
Wine amekuwa akitoa changamoto kubwa kwa Rais wa Muda mrefu wa Uganda Yoweri Museveni mara nyingi akitumia muziki wake kuikosoa serikali na kujipatia wafuasi. Kwa kuhofia uhusiano mzuri wa mwanamuziki huyo na vijana, mamlaka zimekuwa zikitumia vikosi vya usalama kuwazuia wafuasi wake kwa kuwakamata na kutumia mabomu ya machozi, vipigo na kutawanya mikutano yake ya kisiasa.