Manafort aelekea 'kumzamisha' Trump
15 Septemba 2018Msimamo huu mpya wa Manafort unakuja wakati akiamua kukiri makosa ya uhalifu na kuepuka kushitakiwa mara ya pili kwa mashitaka ambayo yangeliweza kumfungisha muda mrefu zaidi jela. Hatua hii inampa mchunguzi maalum, Robert Mueller, mshirika muhimu aliyesimamia juhudi za kuchaguliwa kwa Trump kwenye uchaguzi wa 2016.
Matokeo ya makubaliano hayo yanahakikisha pia kuwa uchunguzi utakwenda mbele zaidi ya uchaguzi wa bunge wa mwezi Novemba licha ya shinikizo kutoka kwa wanasheria wa Rais Trump wanaomtaka Mueller kuachana nao.
Bado haijaeleweka ni taarifa gani kuhusiana na Rais Trump ambayo Manafort anajitayarisha kuwapa wachunguzi au ambayo inaweza kuusaidia uchunguzi wa Mueller juu ya uingiliaji kati wa Urusi kwenye uchaguzi wa 2016.
Lakini ushiriki wake kwenye masuala muhimu yanayochunguzwa na uongozi wake kwenye timu ya kampeni katika wakati ambao waendesha mashitaka wanasema majasusi wa Urusi walikuwa wakifanya kazi ya kuupotosha uchaguzi huo ni mambo yanayoweza kumfanya kuwa shahidi muhimu kabisa.
Makubaliano haya yanamfanya Manafort kuwa mshirika wa karibuni kabisa wa Trump kukiri makosa na kushirikiana na wachunguzi kwa matarajio ya kupunguziwa adhabu.
Kibao chamgeukia Trump
Muda mrefu, Manafort alikuwa amekataa wazo la kutoa ushirikiano huo hata baada ya waendesha mashitaka kuongeza mashitaka dhidi yake mjini Washington na Virginia. Trump aliupongeza msimamo huo hadharani, akisema kuwa "Manafort alikuwa akitendewa vibaya zaidi kuliko jambazi Al Capone." Mwanasheria wa Trump, Rudy Giuliani, alikuwa ameashiria kuwa Manafort angelipewa msamaha baada ya uchunguzi kukamilika.
Lakini ghafla ikaja hatua isiyo kawaida ya siku ya Ijumaa (Septemba 15) ambapo Manafort alikubali kutoa taarifa yoyote atakayoombwa, kutoa ushahidi wakati wowote atakapotakiwa kufanya hivyo na hata kufanya kazi za uchunguzi wa chini kwa chini ikibidi.
Tayari Mueller ameshapata ushirikiano kutoka kwa mshauri wa zamani wa masuala ya usalama aliyelidanganya shirika la ujasusi la FBI juu ya kuzungumzia vikwazo na balozi mmoja wa Urusi, msaidizi wa kampeni aliyeanzisha wazo la kukutana na Rais Vladimir Putin; na msaidizi mwengine aliyeshitakiwa pamoja na Manafort lakini akamgeuka. Mwanasheria wa zamani wa Trump amekiri makosa kwenye uchunguzi mwengine tafauti na huu mjini New York.
Manafort alitiwa hatiani mwezi uliopita kwa makosa manane ya uhalifu wa kifedha katika kesi tafauti mjini Virginia na anakabiliwa na kifungo cha miaka 10 kwa kesi hiyo. Makosa mengine mawili aliyoyakiri siku ya Ijumaa yanaongeza miaka mingine mitano ya kifungo, ingawa hukumu yake inategemea zaidi na kiwango ambacho yuko tayari kutoa ushirikiano.
"Alitaka kuhakikisha kuwa familia yake inaweza kubaki salama na kuishi maisha mazuri. Amekubali kubeba dhamana. Hii ni kwa mambo yaliyotokea siku nyingi nyuma na kila mtu anapaswa kukumbuka hilo," alisema wakili wake, Kevin Downing, nje ya mahakama.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP
Mhariri: Caro Robi