1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mandela bado amelazwa hospitalini

Caro Robi10 Juni 2013

Rais wa zamani wa Afrika kusini Nelson Mandela anasalia hospitalini kwa siku ya tatu baada ya kupata maradhi ya mapafu kwa mara nyingine tena huku serikali ikionekana kuwa kimya kuhusu hali ya shujaa huyo

https://p.dw.com/p/18mey
Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson MandelaPicha: Getty Images

Familia yake ilionekana hapo jana ikitoka katika hospitali moja mjini Pretoria.Hii ni mara ya nne kwa Mandela kulazwa hospitalini tangu mwezi Desemba mwaka jana.Akizungumzia hali yake msemaji wake Mac Maharaj amesema kiongozi huyo anapumua bila usaidizi lakini akasema hali yake si nzuri.

Raia wengi wa Afrika kusini hapo jana walikusanyika makanisani kumuombea Mandela mwenye umri wa miaka 94.Lakini wengi wa raia hao wanaanza kukubali kuwa hata yeye shujaa wao rais wa kwanza mweusi nchini humo ni mwanadamu na lolote laweza mfika.

Gazeti la Sunday Times hapo jana lilikuwa na kichwa cha habari kilicho onyeesha ukweli wa mambo kuwa ni wakati wa kumuacha aende.Rafiki yake wa muda mrefu Andrew Mlangeni mwenye umri wa miaka 87 aliliambia gazeti hilo kuwa wanamtakia Madiba afueni ya haraka lakini anadhani la muhimu ni kwa familia yake kukubali na kumruhusu akapumzike.

Mandela augua
Mandela auguaPicha: picture-alliance/AP

Mlangani ambaye walifungwa na Mandela jela mwaka 1964 ameongeza kuwa punde familia yake ikikubali hilo, watu wa Afrika kusini pia watafuata mkondo na kutoa shukran kwa Mungu kwa kuwapa mtu huyo maishani mwao.

Shujaa wa Afrika alemewa na maradhi

Mandela ambaye anafikisha miaka 95 mwezi ujao anaenziwa si Afrika kusini tu bali bara zima la Afrika na ulimwengu kwa jumla kama kielelezo cha amani na maridhiano kufuatia kuachiliwa kwake kutoka jela alikozuiliwa kwa miaka 27 na kuliunganisha taifa lake kwa kuvunjilia mbali ubaguzi wa rangi nchini humo.

Mapafu ya Mandela yaliharibika akiwa mfungwa alikopata maradhi ya kifua kikuu mwaka 1988.Pia ametibiwa kutokana na saratani ya kibofu cha mkojo na maradhi ya tumbo.Alikuwa akipokea matibabu nyumbani kwake mjini Johannesburg wakati hali yake ilipodhoofika na kupelekwa hospitalini Jumamosi.

Daktari bingwa wa mapafu wa Afrika kusini Guy Richards amesema kujirejea kwa homa ya mapafu ni nadra sana hadi pengine kulikuwa na uharibu wa mapafu hapo mbeleni kwa mfano kama mgonjwa alikumbwa na kifua kikuu basi maeneo yaliyoharibiwa huwa yanashambuliwa na bakteria mara kwa mara.

Mandela na mkewe Graca Machel
Mandela na mkewe Graca MachelPicha: picture-alliance/dpa

Homa ya mapafu yamkuba tena

Mwezi desemba alilazwa hospitalini kwa siku 18.Baadaye mwezi Machi mwaka huu alilazwa tena na mwishoni mwa mwezi huo huo alilazwa kwa siku 10 akiugua homa ya mapafu.

Mkewe Bi Graca Machel amekuwa kando ya kitanda chake hospitalini baada ya kukatisha ziara mjini London Uingereza.Bintiye Zindzi hapo jana alimtembelea babake hospitalini na kusema ni shujaa.

Viongozi kutoka kwingine duniani akiwemo waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na afisi ya Rais wa Marekani Barrack Obama wametuma risala za kumtakia afueni ya haraka huku wapenzi wake wakimiminia ujumbe wa heri katika mitandao ya kijamii kutoka kila pembe ya dunia.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Josephat Charo.