1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mane aizamisha Misri tena na aibandua nje ya Dimba la Dunia

30 Machi 2022

Nyota wa timu ya Liverpool Sadio Mane aliiongoza timu yake ya taifa Senegal kukata tiketi ya kushiriki kinyang'anyiro cha kuwania Kombe la Dunia.

https://p.dw.com/p/49Dk2
WM-Qualifikationsspiel Senegal - Ägypten
Picha: Stefan Kleinowitz/AP Photo/picture alliance

Kando na Senegal, timu nyingine za Afrika ambazo zimetinga fainali za Kombe la Dunia mjini Doha huko Qatar ifikapo Novemba na Disemba mwaka huu ni pamoja na Cameroon, Ghana, Morocco na Tunisia.

Senegal waliibuka washindi dhidi ya miamba wa Afrika Misri bao 1-0, katika muda wa kawaida ikiwa ni mechi ya marudio mjini Diamniadio.

Katika mechi yao ya kwanza, Misri waliibuka washindi kwa bao 1-0. Kwa hivyo walikuwa sare bao 1-1, katika muda wa ziada, hatimaye ikawa ni mikwaju ya penalti.

Soma pia: Misri yapanga kulipiza kisasi dhidi ya Senegal

Kama ilivyokuwa katika michuano ya kuwania kombe la ubingwa barani Afrika mwezi uliopita, hata jana, Sadio Mane alipewa nafasi na timu yake kupiga mkwaju wa mwisho wa penalti, na kwa mara nyingine hakubahatisha bali alicheka na nyavu. 

Mohamed Salah wa Misri ambaye pia hucheza na Sadio mane katika timu ya Liverpool, alishindwa kufunga penalti, pale kombora lake lilienda juu ya mtambaa-panya. Matokeo yakawa ni ushindi wa mabao 3-1.
Mohamed Salah wa Misri ambaye pia hucheza na Sadio mane katika timu ya Liverpool, alishindwa kufunga penalti, pale kombora lake lilienda juu ya mtambaa-panya. Matokeo yakawa ni ushindi wa mabao 3-1.Picha: Stefan Kleinowitz/AP Photo/picture alliance

Huku Senegal ikishangilia kufuzu kwao mara ya pili mfululizo kuwania kombe la dunia, Misri ambao ni miongoni mwa miamba ya soka Afrika walibaki na simanzi ya kushindwa mara mbili na Senegal mwaka huu.

Lakini si Misri pekee ambao ni magwiji waliotupwa nje. Super Eagles ya Nigeria pia hawatashiriki dimba hilo la Qatar mwaka huu baada ya kubanduliwa na majirani wao Ghana.

Soma pia: Droo ya Kombe la Dunia kufanyika Qatar

Ghana walitoka sare ya bao 1-1 na Nigeria nchini Nigeria,  lakini maadamu Ghana walifunga bao ugenini walijikatia tiketi. Bao la Ghana lilifungwa na kiungo wa kati wa Arsenal Thomas Partey mnamo dakika ya kumi.

Wafanyakazi wa umma wa Nigeria walikuwa wamepewa nafasi ya kufanya kazi nusu ya siku kusudi waweze kuishangilia timu yao, na vilevile mashabiki walipewa usafiri wa bure ili kuujaza uwanja wa Abuja ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 60,000. 

Katika mechi kati ya Cameroon na Algeria, Cameroon walishinda, na kujikatia tiketi kuwania kombe la dunia. Mchuano huo uliojaa patashika, uliwaacha mashabiki wengi na masimulizi.
Katika mechi kati ya Cameroon na Algeria, Cameroon walishinda, na kujikatia tiketi kuwania kombe la dunia. Mchuano huo uliojaa patashika, uliwaacha mashabiki wengi na masimulizi.Picha: Bouhara Hamza/ABACA/picture alliance

Mnamo dakika ya nne ya muda wa nyongeza mechi ikikaribia kuisha, mabao kwa wakati huo yakiwa 1-1, Karl Ekambi aliifungia timu yake Cameroon bao na kufanya mambo kuwa 2-1 mjini Blida.

Katika mechi yao ya kwanza Algeria waliibuka kidedea kwa bao 1-0.  Mwisho wa yote matokeo yakawa ni 2-2, Cameroon ikajikatia tiketi kwa msingi wa mabao ya ugenini. 

Soma pia: Infantino: Kombe la dunia la Qatar 2022 litakuwa kivutio

Kwingineko, Morocco walijikatia tiketi baada ya kuinyuka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mabao 4-1 mjini Casablanka. Hii itakuwa mara ya sita kwa Morocco kutinga fainali za kombe la dunia.

Tunisa nao wakiwa mbele ya mashabiki wao, walijikatia tiketi ya dimba la Qatar baada ya kutoka sare ya 0-0 na dhidi ya Mali, mechi ya marudio.

Katika mechi yao ya kwanza ugenini, Tunisia walitoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mali.

(AFPE)