1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manung'uniko katika klabu ya Bayern

29 Januari 2016

Kuna ripoti za kuwapo mvutano katika kikosi cha BAYERN MUNICH ambapo jarida la michezo la Ujerumani Kicker limemnukuu mchezaji mmoja akisema kuwa mazingira siyo mazuri kabla ya kuondoka kwa Pep Guardiola

https://p.dw.com/p/1Hm09
Fußball Bundesliga FC Bayern München - Hamburger SV Jerome Boateng Verletzung
Picha: picture alliance/Laci Perenyi

Bayern iko katika uongozi wa msimamo wa Bundesliga ambapo wana pengo la pointi nane mbele ya nambari mbili Borussia Dortmund na wanaelekea kushinda taji lao la nne mfululizo la Bundesliga.

Lakini nje ya uwanja, kuna uvumi kuwa Guardiola ana uhusiano mbaya na wachezaji baada ya kutangaza mwezi jana kuwa ataondoka mwishoni mwa msimu baada ya kuwa katika klabu hiyo kwa miaka mitatu.

Mhispania huyo amesema anataka kufunza nchini England msimu ujao lakini anataka kuondoka kwa kuipa Bayern mataji matatu, Bundesliga, Champions League na Kombe la Shirikisho – DFB Pokal.

Lakini Guardiola mwenye umri wa miaka 45 amekumbwa na shinikizo baada ya beki Jerome Boateng kuwa mchezaji wa 14 kuumia msimu huu. Wachezaji Mario Goetze, Mehdi Benatia, Rafinha na Franck Ribery wanauguza maumivu. Juan Bernat na Javi Martinez wamerejea kikosini. Arjen Robben aliiambia televisheni moja ya Uholanzi kuwa alikasirishwa na hatua ya Guardiola kuondoka.

Jarida la michezo la Kicker limeripoti kuwa mtu mmoja katika kikosi hicho amezusha mgawanyiko kwa kukiti kuwa mazingira siyo mazuri kikosini wakati kocha Pep Guardiola akiimariha udhibiti wake. Mtu huyo ameliambia jarida hilo la Ujerumani kuwa kikosi hakijafurahishwa baada ya kutumiwa barua pepe, ambayo inasema lazima sasa watoe habari rasmi kuhusiana na safari zao katika siku ambazo wako mapumzikoni ili kuepusha safari zozote zisizo za msingi. Hata hivyo Guardiola amepuuza ripoti hizo akisema kuwa kila kitu kiko shwari katika kikosi chake.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/reuters
Mhariri: Daniel Gakuba