1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maombi ya dua kwa marehemu Khashoggi yaanza leo

16 Novemba 2018

Uturuki imesema ina ushahidi zaidi kuhusiana na mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi, kauli ambayo inatofautiana na ile ya Saudi Arabia, limesema gazeti moja la Uturuki.

https://p.dw.com/p/38N3m
Jamal Khashoggi
Picha: Getty Images/C. McGrath

Kwenye Chapisho moja la gazeti hilo, inaeleza kuwa ushahidi huo ni rekodi ya pili ya sauti ya siku ambayo Khashoggi aliuawa. Kulingana na gazeti hilo la Hurriyet, rekodi hiyo ya sauti inayodaiwa kuwa ya urefu wa dakika kumi na tano, inadhihirisha kwamba mauaji ya Khashoggi yalipangwa.

Taarifa hiyo inatofautiana na Mkuu wa Mashtaka wa Saudi Arabia Saud al-Mojeb ambaye jana Alhamisi alisema kwamba maafisa watano wa Saudi wanakabiliwa na adhabu ya kifo, kwa kosa la mauaji ya mwandishi huyo, lakini ikamwondolea lawama Mwanamfame Mohammed bin Salman.

Miongoni mwa maafisa watano waliofutwa kazi na Mwanamfalme bin Salman ni aliyekuwa naibu mkuu wa upelelezi, Ahmed al-Asiri, ambaye pia aliwahi kuwa karibu sana na bin Salman. Khashoggi mwenye umri wa miaka 59, ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Mwanamflame, aliuliwa na mwili wake kukatwakatwa katika ofisi ndogo ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul tarehe 2 Oktoba mwaka huu.

Saud al-Mojeb Staatsanwalt Saudi-Arabien
Mkuu wa Mashtaka wa Saudi Arabia Saud al-MojebPicha: picture-alliance/AP Photo/DHA

Uturuki imesema mauaji hayo yalitekelezwa na kundi la raia wa Saudi Arabia ambao walisafiri kuelekea Istanbul kwa lengo hilo. Rais wa Uturuki Reep Tayyip Erdogan agizo hilo lilitolewa na uongozi wa juu wa serikali ya Saudi Arabia, lakini hakumtaja Mwanamfalme Salman moja kwa moja.

Kwenye gazeti hilo la Uturuki, Hurriyet, mwandishi Abdulkadir Selvi, anadai kuwa rekodi ya kwanza ya sauti inathibitisha kuwa Khashoggi alinyongwa lakini rekodi ya pili iliyorekodiwa kabla ya Khashoggi kuingia katika ubalozi huo, inaonesha wazi kuwa mauaji hayo yalipangwa awali.

Ameongeza kuwa kanda ya pili inathibitisha kuwa watu kumi na tano walikuwa ndani ya ubalozi huo kabla ya mwanahabari huyo kufika na walikuwa wakijadiliana kuhusu jinsi watakavyotekelza mauaji yake.

Fall Khashoggi - Gedenkveranstaltung in Washington
Picha: picture-alliance/AP/J.S. Applewhite

Uturuki pia ina ushahidi kwamba kundi hilo lilipiga simu za kimataifa baada ya mauaji. Wakuu wa mashtaka nchini Saudi Arabia jana walitangaza kuwa iliwafungulia mashtaka watu 11 na kusema jumla ya watu 21 wanazuiliwa kwa kuhusishwa na mauaji ya Khashoggi.

Wakati hayo yakijiri, mwanawe wa kiume wa Khashoggi, kupitia mtandao wake wa Twitter, amesema maombi ya dua kumuombea marehemu baba yake yatafanyika nyumbani kwa marehemu mjini Jeddah kuanzia leo Ijumaa hadi Jumapili.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman