1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Chama cha mrengo mkali wa kulia chashinda Brazil

9 Oktoba 2018

Nchini Brazil chama cha Social Liberal PSL kinachoelemea siasa kali za mrengo wa kulia kimepata ushindi katika duru ya kwanza, kikikosa chupuchupu kupata ushindi wa moja katika uchaguzi huo wa rais.

https://p.dw.com/p/36DR0
Brasilien Wahl 2018 | Stimmabgabe Jair Bolsonaro
Picha: imago/Xinhua/T. Ribeiro

Baada ya miaka minne ya mgogoro katika taifa hilo, wapiga kura mnamo siku ya Jumapili walivuruga kabisa nafasi ya kuanzishwa sura mpya ya historia ya Brazil. Waliwapa fursa kwa urahisi wagombea wawili ambao wana ushawishi mkubwa kwa watu kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi na hivyo ni sawa na kuongeza matatizo yanayoikabili nchi hiyo.

Jair Bolsonaro wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha (PSL) amefanikiwa kushinda kwa asilimia 46 katika duru ya kwanza kwenye ya uchaguzi huo wa rais. Nafasi ya pili imechukuliwa na meya wa zamani wa Sao Paulo, Fernando Haddad wa chama cha PT kinacholemea mrengo wa shoto kwa kupata asilimia 29.

Kushoto:Jair Bolsonaro Kulia:Fernando Haddad
Kushoto:Jair Bolsonaro Kulia:Fernando HaddadPicha: Reuters/P. Whitaker/N. Doce

Hadad aligombea badala ya rais wa zamani wa Brazil Luiz Inacio da Silva, anayejulikana kwa jina la utani Lula, na ambaye yumo jela baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na rushwa na hivyo kuzuiwa kugombea katika kinyang'anyiro hicho.

Mgogoro huu mkubwa wa kisiasa nchini Brazil umeibuka kutokana na mchanganyiko wa mambo ambayo yamegeuka na kuwa majeraha katika jamii tangu mwaka 2013. Katika mwaka huo, mamilioni ya watu waliandamana mabarabarani kupinga rushwa, ongezeko la nauli katika usafiri wa umma na gharama kubwa ya ujenzi wa viwanja vilivyotumika katika mashindano ya Kombe la Dunia.

Siasa za jadi nchini Brazil za chama cha PT hazikufaulu kutoa majibu ambayo labda yangesaidia kurudisha imani ya wapiga kura. Mfumo wa siasa wa chama hicho ulitetereka kwanza kwa kuondolewa madarakani rais wa zamani Dilma Rousseff kwa makosa ya uhalifu na kisha kuunga mkono serikali ya rais Michel Temer ambaye hapendwi. Na sasa kimeshindwa kumteua mgombea ambaye angeweza kuwashawishi wapiga kura wa kihafidhina.

Rais wa zamani wa Brazil Lula da Silva
Rais wa zamani wa Brazil Lula da SilvaPicha: picture-alliance/Zuma Press/P. Lopes

Kutokana na matokeo ya kura katika duru ya kwanza, ishara zote zinaonyesha kwamba vyama vya kizalendo vinavyolemea mrengo mkali wa kulia vitashinda katika uchaguzi wa marudio mnamo tarehe 28 Oktoba. Mwandishi Francis Franca wa DW anauliza ikiwa makubaliano juu ya maadili ya pamoja ni dhaifu mno katika jamii hii, ni ipi nafasi ya wanademokrasia dhidi ya watu wanaounga mkono vyama vya mrengo mkali wa kulia?

Mwandishi:Zainab Aziz/Francis Franca/ LINK: http://www.dw.com/a-45794149

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman