Maoni: China yakomesha utawala wa demokrasia Hong Kong
12 Machi 2021Mwandishi wa DW Dang Yuang katika maoni yake haya anasema hivi sasa kwenye eneo hilo, hakuna demokrasia tena, bali mfano tu wa demokrasia yenyewe.
Sehemu ya utangulizi wa katiba ya China, unaitaja nchi hiyo kama taifa la watu la demokrasia ya kidikteta linaloongozwa na wafanyakazi.
Mfumo wake wa uchumi wa sasa ni " wa soko la kisoshalisti” ambao una mchanganyiko wa umiliki binafsi wa masoko na jukumu la pamoja yaani ujamaa. Kwa suala la Hong Kong, walileta kile walichokiita "taifa moja, mifumo miwili,". Kwa maana ya utawala wa Hong Kong kwa ajili ya watu wa Hong Kong, "na kiwango cha juu cha kujitawala" — hii ikiwa ni kanuni zilizokubaliwa na China na Uingereza kabla ya eneo hilo lililokuwa chini ya utawala wa Uingereza kukabidhiwa kwa China mnamo mwaka 1997.
Kanuni hizi zilizaa sheria ya msingi ya Hong Kong, inayokidhi viwango vya kimataifa vya demokrasia. Hata hivyo sheria hii ya msingi, ina sehemu inayovutia: Inaelekeza uchaguzi wa moja kwa moja na uchaguzi mkuu kuchagua wabunge wa Hong Kongna mtendaji mkuu wa jimbo hilo, lakini iko kimya kuhusu muda wa uchaguzi huo kufanyika. Hii imeipa nafasi China kucheza na mwanya huo.
Ni kweli, uchaguzi hufanyika Hong Kong lakini wakati wote nyuma ya pazia huwa na nguvu yenye ushawishi isiyofahamika, na nguvu hiyo hufika kila mahali. Hutaka kudhibiti kila kitu ili kuzuia ukosoaji wa aina yoyote. Na nguvu hii si nyingine bali ni Chama cha Kikomunisti cha China (CCP).
Mfumo wa uchaguzi wa wawakilishi wa HongKong
Tangu Hong Kong ilipowekwa chini ya udhibiti wa China, nchi hiyo imekuwa ikizuia uhuru wa walio wengi katika jimbo hilo. Takribani nusu ya wabunge 70 wa eneo hilo huchaguliwa moja kwa moja na watu wa Hong Kong; nusu nyingine, huteuliwa na jumuiya na makundi ya kijamii yaliyoandaliwa. Uchaguzi wa kiongozi wa jimbo hilo ni lazima athibitishwe na tume yenye uhusiano mzuri na China.
Azimio lililopitishwa alhamisi na baraza la taifa kwa kura 2,895 linasema wagombea wote katika uchaguzi ujao wa bunge, na wale wa kiongozi wa jimbo hilo watachujwa na kuthibitishwa na tume ile ile yenye uhusiano mzuri na china. Hii ni kuhakikisha wagombea wote wa nafasi za uongozi ni "wazalendo”.
Kwa hivyo siyo wale wanaoipenda Hong Kong bali wanaopenda utawala wa kidikteta. Kwa maana hiyo, kwa msimamo wa China, vyama vya upinzani vinavyounga mkono demokrasia, havipo upande wa wazalendo.
Mwandishi: Dang Yuang
Tafsiri: Angela Mdungu
Mhariri: Mohammed Khelef