1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi yanapopigana na madola

Alexander Kudascheff16 Novemba 2015

Wanaoitwa wapiganaji wa jihadi wanataka kuushinda ulimwengu wa kisasa, imani na jamii ya kidemokrasia kwa kutangaza vita vya muda mrefu, anasema Mhariri Mkuu wa Deutsche Welle, Alexander Kudascheff.

https://p.dw.com/p/1H6M3
Waumini kwenye kanisa la Notre Dame mjini Paris wakifanya ibada ya kuwaombea waliouawa.
Waumini kwenye kanisa la Notre Dame mjini Paris wakifanya ibada ya kuwaombea waliouawa.Picha: Reuters/L. Bonaventure

Baada ya mashambulizi ya kigaidi mjini Paris, wengi wetu tunajihisi kuelemewa na hisia kwamba dunia imeng'oka kwenye kiungo chake, kwamba mfumo wa kilimwengu unaporomoka. Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, amefikia umbali wa kuzungumzia Vita vya Tatu vya Dunia.

Hii haimaanishi vita vya ulimwengu, lakini vita hivi vinapiganwa dhidi ya dunia tunayoijuwa sisi. Vita hivyo vimetangazwa na imani ya vita vitakatifu sio tu na utawala uliojitangaza wenyewe kuwa ni "Dola la Kiislamu", bali pia na makundi mengi mengine yanayofuata siasa kali za kidini duniani. Vita vyao sasa vinavuuka mipaka na kuingia Ulaya na vinaipa changamoto dunia.

Hata hivyo, kutokana na sababu za kimkakati, vita hivi vinakosa uwiano kwa kiasi kikubwa sana. Wachache wanapambana dhidi wengi, watu wa kawaida dhidi ya mataifa. Ni mapambano ya wanamgambo binafsi wa Kiislamu dhidi ya majeshi ya madola.

Mhariri Mkuu wa DW, Alexander Kudascheff.
Mhariri Mkuu wa DW, Alexander Kudascheff.

Msingi wa vita hivi

Msingi wake ni mmoja tu. Dola linapaswa kufanya chochote kuwazuwia magaidi wasifanikiwe. Linapaswa kufanya kila kitu kuhakikisha kwamba raia wake wanaishi kwa usalama – kila saa, kila siku, kila mwezi, kila mwaka, na mahala popote walipo. Magaidi kwa upande wao wanataka ushindi mmoja tu – wanahitaji shambulizi moja tu lililofanikiwa kuyachanganya madola kama ilivyotokea tarehe 13 Novemba mjini Paris.

Vita hivi pia havina uwiano kwa sababu pande mbili zilizo kwenye vita vyenyewe zinafanya kazi chini ya masharti na hali tafauti. Kwa upande mmoja, una wapiganaji wa siasa kali ambao wanayaangamiza maisha yao wenyewe; kwa upande mwengine, una polisi na wanajeshi ambao wanafanya kazi kwa kuzingatia hoja na uhalisia.

Huku kuna utayarifu wa kuvuuka mipaka yote na kutumia njia za kikatili zaidi zinazowezekana, hule kuna wanajeshi na polisi ambao wanafanya kazi kwa mujibu wa misingi ya kikatiba. Wao wanafungwa na sheria, wapiganaji wa siasa kali wanaongozwa na itikadi yao ya kikatili.

Utayarifu wa kufanya mauaji ya kikatili unasimama mbele ya misingi ya kidemokrasia na yale yote ambayo demokrasia inayatukuza. Ni vita visivyo na uwiano, hata kama ulimwengu wa Magharibi utalazimika kufikiria tena sera yake ya kimsingi juu ya usalama.

Mwandishi: Alexander Kudascheff
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo